Sadifa Juma Hamisi
Arusha.
Wakati joto la urais likizidi kupanda ndani ya CCM kutokana na hofu ya
baadhi ya majina mazito ya wagombea wa nafasi hiyo kukatwa kwa mizengwe,
vita vya wagombea sasa ni dhahiri baada ya mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM
kusema hakuna mtu atakayekatwa bila ya sababu za msingi.
Mjumbe
huyo, Sadifa Juma Hamisi, ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM), pia alisema umoja huo haujafikia uamuzi wala kumtuma mtu
kumdhibiti mwanachama anayetajwa kuwania urais.
Katika
siku za karibuni kumekuwapo mjadala mkubwa ndani ya CCM juu ya mtu
atakayepitishwa kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho, na ilizidi
baada ya Rais Jakaya Kikwete kueleza kuwa mwanachama ambaye atateuliwa
na CCM kugombea urais hayumo miongoni mwa waliojitokeza na kuwataka
wanachama kuwashawishi watu wenye sifa wajitokeze.
Siku
chache baadaye, Dk Raphael Chegeni aliliambia gazeti la Mwananchi kuwa
ametumwa na wanachama wa CCM wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda
kumshawishi Lowassa kujitokeza kuwania urais kuitikia wito wa Rais
Kikwete wa kuwataka wanachama kuwashawishi watu wenye sifa kujitokeza.
Hadi
sasa, wanachama waliojitokeza kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais ni
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, January Makamba (Naibu Waziri wa Sayansi na
Teknolojia), Hamisi Kigwangala, na Lazaro Nyalandu ambaye ni waziri wa
Maliasili na Utalii.
Lakini
pia wako wanaotajwa kuwania urais lakini hawajatangaza ambao ni Waziri
wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sita, William Ngeleja,
Emmanuel Nchimbi, Mwigulu Nchemba, Stephen Wasira, Bernard Membe na
Edward Lowassa ambaye ameibua mjadala kati ya kambi yake na
zinazompinga.
Mapema
wiki iliyopita, katibu wa uhamasishaji na chipukizi wa UVCCM, Paul
Makonda alikaririwa akisema kuwa vitendo vyake vya kumshambulia Lowassa
vinatokana na kutumwa na umoja huo kumdhibiti, jambo ambalo limezidisha
mjadala kuhusu mteule wa chama hicho.
Kutokana
na hofu hiyo, viongozi wa UVCCM na CCM mkoani Arusha wametuma ujumbe wa
maneno kwa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa za chama hicho
wakitaka wanachama wasifanyiwe kile wanachokiita kuchafuana na vitisho
vya baadhi ya wagombea kukatwa kimizengwe.
Ujumbe
huo ulitumwa juzi na mwenyekiti wa CCM wa mkoa, Onesmo ole Nangole na
mwenyekiti wa UVCCM, Robinson Meitinyiku ambao walitaka Sadifa Juma
Hamis kueleza msimamo wa mkoa kwa vyombo hivyo viwili vya maamuzi, na
mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM aliwahakikishia kuwa hakuna mgombea
atakayekatwa kwa "sababu za kijinga".
Akijibu
ujumbe wa viongozi hao, Sadifa aliyekuwa jijini hapa kumsimika kamanda
wa vijana wa wilaya ya Arumeru, Mathias Manga, aliwaondolea hofu katika
hafla hiyo akisema hakuna mgombea wa urais wa CCM ambaye atakatwa bila
sababu za msingi, lakini akawataka vijana kusubiri zamu yao hadi 2025.
Kauli ya Sadifa
"Niwaombeni
mwenyekiti wa mkoa na mwenyekiti wa UVCCM, msiogope. Hakuna mtu
atakayekatwa kijinga ndani ya Kamati Kuu au Halmashauri Kuu. Kikubwa
tufuate maadili. Mimi mchapakazi ndiye nitamtetea," alisema bila kutaja
mgombea anayekusudiwa.
Alisema
ni lazima kiongozi bora awe na mikakati na dira na upeo wa kuwa na
mikakati bora ya kutekeleza ahadi zake kwani hatuwezi kuwa na kiongozi
ambaye hana dira wala mikakati.
"Tunataka
kiongozi mwenye kujiamini, awe ana vision (dira) na mission (mikakati),
msikivu... hatuwezi kuchagua rais ambaye hana sifa hizi," alisema.
Akizungumzia
maombi ya Nangole kuhusu tabia ya kuwachafua baadhi ya wagombea na
kuwatisha, Sadifa alisema hakuna kiongozi aliyetumwa na CCM na UVCCM
kutukana mtu wala kumtisha.
"Mzee
wangu, watu wengi wanajua wanamtaka nani, ukiona mtu anapanda kwenye
majukwaa anamchafua mwenzake, ujue huyo ana mapungufu ya malezi, hakuna
haja ya kumjibu kwani utaonekana na pia wewe una mapungufu," alisema.
Akionekana
kujibu kauli ya Makonda, Sadifa alisema UVCCM haijatuma mtu amtukane
mwingine. Alisema akiwa mjumbe wa Kamati Kuu, hawajawahi kumtuma
kiongozi yoyote kumtukana mwanachama mwingine wa CCM.
Alipoulizwa
kuhusu hofu hiyo, kwa kifupi katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape
Nnauye alisema: "Mimi siwezi kuwa msemaji wa Umoja wa Vijana, nikisema
niwajibu nitakuwa nimepotoka."
Mapema
wiki iliyopita, Makonda alikaririwa akisema kuwa amekuwa akimshambulia
Lowassa, ambaye anatajwa kuwania urais kupitia CCM, kwa sababu ametumwa
na umoja huo.
Makonda
amekuwa akikaririwa mara kwa mara akisema kuwa Lowassa hafai kuwa mteule
wa CCM wa kuwania urais na mikanda ya kauli zake imesambaa kwenye
mitandao ya kijamii, jambo lililofanya uteuzi wake kuwa Mkuu wa Wilaya
ya Kinondoni uhojiwe na watu wengi na hivyo kujikuta akilazimika kusema
ametumwa na umoja wake kumdhibiti waziri mkuu huyo wa zamani.
Katika
mazungumzo yake juzi, Sadifa hakutaka kutaja jina la mgombea
atakayemtetea wala mtu anayemshambulia, badala yake alisema muda
ukifika, kila kitu kitajulikana kwa kuwa watu wanamjua mgombea
wanayemtaka.
"Mwenyekiti,
dawa ya mjinga ni kukaa kimya, watu wanamjua mtu ambaye wanamtaka. Rais
Jakaya Kikwete ni mtu ambaye hatabiriki, hana ushemeji... nyie subirini
tu wakati ukifika," alisema.
Vijana na urais
Akizungumzia vijana ambao wanautaka urais, Sadifa aliwataka kusubiri zamu yao hadi 2025 ili wazee waliopo wamalize muda wao.
Alisema
utakapofika mwaka 2025 vijana watakuwa katika nafasi nzuri sana ya
kushika uongozi na hawatakubali kuona viongozi wazee wakitaka kupewa
nafasi.
"Wazee tutawaomba radhi mwaka wenu ni 2015 hadi 25, mkimaliza hapo, miaka yenu imekwisha, msije tena," alisema.
Kauli ya Nangole
Awali,
Nangole, ambaye aliwahi kusema kuwa Lowassa ni kiongozi msikivu na
makini na ambaye ni tegemeo la Watanzania katika kuwaunganisha kuwa kitu
kimoja, aliomba Kamati Kuu ipelekewe ujumbe kuwa CCM mkoani Arusha
hairidhishwi na matendo ya baadhi ya viongozi kuwatukana na kuwatisha
wengine.
Nangole
alirejea kauli aliyowahi kuitoa kuwa CCM ni ya wanachama wote na ndani
yake hakuna sisimizi au tembo wa kumtisha mwingine ili mradi anafuata
taratibu za chama hicho.
Alisema
imeibuka tabia ya baadhi ya viongozi wa CCM, kuwatisha wengine na
kuwatukana kana kwamba wao ndio wana hatimiliki ya CCM.
Naye
mwenyekiti wa UVCCM mkoani Arusha, Robinson Meitinyiku alisema kuna
kiongozi mmoja ametoa kauli kuwa mgombea mmoja hata kama akisafishwa na
madodoki hawezi kuwa msafi.
Badala
yake alisema kiongozi aliyetoa maneno hayo ndiye hawezi kusafishika hata
kwa gunzi kwani kuna taarifa aliwahi kusaliti na kujiunga na chama
kingine.CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment