Sadifa Juma Hamisi
Arusha.
Wakati joto la urais likizidi kupanda ndani ya CCM kutokana na hofu ya
baadhi ya majina mazito ya wagombea wa nafasi hiyo kukatwa kwa mizengwe,
vita vya wagombea sasa ni dhahiri baada ya mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM
kusema hakuna mtu atakayekatwa bila ya sababu za msingi.
Mjumbe
huyo, Sadifa Juma Hamisi, ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM), pia alisema umoja huo haujafikia uamuzi wala kumtuma mtu
kumdhibiti mwanachama anayetajwa kuwania urais.
Katika
siku za karibuni kumekuwapo mjadala mkubwa ndani ya CCM juu ya mtu
atakayepitishwa kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho, na ilizidi
baada ya Rais Jakaya Kikwete kueleza kuwa mwanachama ambaye atateuliwa
na CCM kugombea urais hayumo miongoni mwa waliojitokeza na kuwataka
wanachama kuwashawishi watu wenye sifa wajitokeze.
Siku
chache baadaye, Dk Raphael Chegeni aliliambia gazeti la Mwananchi kuwa
ametumwa na wanachama wa CCM wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda
kumshawishi Lowassa kujitokeza kuwania urais kuitikia wito wa Rais
Kikwete wa kuwataka wanachama kuwashawishi watu wenye sifa kujitokeza.
Hadi
sasa, wanachama waliojitokeza kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais ni
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, January Makamba (Naibu Waziri wa Sayansi na
Teknolojia), Hamisi Kigwangala, na Lazaro Nyalandu ambaye ni waziri wa
Maliasili na Utalii.
Lakini
pia wako wanaotajwa kuwania urais lakini hawajatangaza ambao ni Waziri
wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sita, William Ngeleja,
Emmanuel Nchimbi, Mwigulu Nchemba, Stephen Wasira, Bernard Membe na
Edward Lowassa ambaye ameibua mjadala kati ya kambi yake na
zinazompinga.
Mapema
wiki iliyopita, katibu wa uhamasishaji na chipukizi wa UVCCM, Paul
Makonda alikaririwa akisema kuwa vitendo vyake vya kumshambulia Lowassa
vinatokana na kutumwa na umoja huo kumdhibiti, jambo ambalo limezidisha
mjadala kuhusu mteule wa chama hicho.
Kutokana
na hofu hiyo, viongozi wa UVCCM na CCM mkoani Arusha wametuma ujumbe wa
maneno kwa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa za chama hicho
wakitaka wanachama wasifanyiwe kile wanachokiita kuchafuana na vitisho
vya baadhi ya wagombea kukatwa kimizengwe.