Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete
Rais wa
Tanzania Jakaya Kikwete amekutana na Viongozi wa Chama cha Watu wenye
Albino Tanzania na kuahidi kufanya kila liwezekanalo kuongeza nguvu ili
kumaliza tatizo la amauaji ya dhidi ya Albino.
"Mauaji
haya yanaisikitisha Serikali na kuifedhehesha sana, msidhani hatufanyi
lolote, tunafanya juhudi kubwa na mbalimbali lakini imefikia wakati
tuongeze juhudi hizo"alisema Rais.
Katika
kikao hicho viongozi wa watu wenye Albino nchini wamesoma risala ambayo
imetoa kilio chao na mapendekezo yao kwa serikali na hatimaye ikaafikiwa
kuwa na haja ya kuunda kamati ya pamoja ambayo itajumuisha Serikali,
viongozi wa watu wenye Albino, viongozi wa waganga wa jadi na wadau wote
wakuu katika suala hili ili kupata mapendekezo na mkakati wa pamoja
ambao hatimaye mauaji haya kukomeshwa kabisa nchini Tanzania.BBC
Rais Kikwete akizungumza na wawakilishi kutoka Chama cha Albino Tanzania
Rais
Kikwete amesema mauaji ya watu wenye Albino hayafanywi na Serikali bali
watu ambao wako katika jamii zetu kwa kushirikiana na waganga wa jadi na
watu wengine wenye tamaa mbalimbali katika jamii hivyo ni lazima
yakomeshwe.
"Kwenye
familia, jamii na hatimaye vyombo vya ulinzi na usalama na hilo ndiyo
jukumu kubwa ambalo Serikali inapaswa kulisimamia na tutalisimamia kwa
ushirikiano wa pamoja". Rais amesisitiza na kuongeza kuwa kamati hiyo ya
pamoja itaweka mikakati ya kuwabaini wale wote wanaohusika kuanzia
wakala, waganga na hatimaye wale wanaonufaika na viungo vya watu wenye
Albino.
Rais
Kikwete pia amesema Serikali itasaidia familia na wahanga wa vitendo vya
mauaji kwa hali na mali ili waweze kujimudu na pia kuwapa ushauri
nasaha ili kuondokana na majonzi yanayosababishwa na vitendo hivyo kwani
vinawaletea waathirika na watu wanaoishi na Albino mfadhaiko na msongo
wa mawazo katika jamii na hivyo kushindwa kuendelea na maisha yao ama
kufanya shughuli zao za kila siku.
Jamii ya Albino imekuwa mashakani kutokana na vitendo vya mauaji vinavyosababishwa na imani za kishirikina
Katika
kikao cha leo, viongozi wametoa kilio chao kwa serikali kuziangalia na
kuzimulika taasisi zisizo za kiserikali ambazo pamoja na kujipambanua
kuwa zinatetea haki za watu wenye Albino nchini bado hazina mkakati wa
pamoja na hazipo wazi kwa walengwa hapa nchini.
Mapema
leo asubuhi mara baada ya kufika Ikulu, kulitokea sintofahamu baina ya
viongozi wa Chama cha Watu Wenye Albino na watu wasio wanachama kwa kile
kilichoelezwa kuwa uongozi huo sio halali kwa vile muda wake
umeshakwisha wa kukaa madarakani.
Hata
hivyo Mwenyekiti wa Chama cha Albino, Ernest Kimaya ameelezea masikitiko
kwake kwa Rais na kuelezea kuwa uchaguzi haukuweza kufanyika kutokana
na ukosefu wa fedha na wamemuomba Rais awasaidie kutimiza azma yao ya
kuitisha mkutano na kuchagua viongozi wa Chama chao.
Kulingana
na Bw. Kimaya wamepanga kufanya mkutano huo wa kuchagua viongozi
katikati ya mwaka huu ambapo pia dunia itakua inaazimisha siku ya watu
wenye Albino duniani.
Rais amekubali ombi hilo na hiyo itazungumzwa kwa urefu katika kamati ya pamoja ambayo inatarajiwa kuwa imekamilika wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment