Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli
Siha. Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli
ameagiza kwa kusimamishwa kazi aliyekuwa kigogo wa Kituo cha Kimataifa
cha Mikutano Arusha (AICC) ambaye hafanyi kazi tena kituoni hapo.
Agizo hilo alilitoa juzi, huku akitaka pia
mkurugenzi wa zamani wa majengo na miradi wa AICC, Paul Ndossa ambaye
awali akifanya kazi Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) akiwa mtaalamu na
mshauri, asimamishwe.
Wakati Dk Magufuli akitoa agizo hilo, Ndossa alikuwa ameshaondoka AICC tangu Januari.
Agizo hilo lilitokana na Mtendaji Mkuu wa TBA,
Elius Mwakifugile kudai kuwa Ndossa ndiye aliyesimamia ujenzi wa majengo
ya ofisi za wakuu wa wilaya za Siha na Moshi.
Majengo hayo mawili yanadaiwa kugharimu mabilioni
ya shilingi, lakini yalijengwa chini ya kiwango tangu yalipokamilika
miaka mitano iliyopita na hayafai kwa matumizi ya kiofisi.
Hata hivyo, Ndossa alipotafutwa kuzungumzia madai hayo alishangazwa na kutuhumiwa kuwa alikuwa mtaalamu mshauri wa miradi hiyo.
Ndossa alisema waziri atakuwa amepewa taarifa potofu.
“Mimi sikuwa consultant (mtaalamu mshauri) wa
ujenzi wa hilo jengo (la Siha). Consultant wa mradi walikuwa TBA, Makao
Makuu...waliitumia ofisi ya Kilimanjaro mimi sikuwa Moshi.
“Nilikuwa nakwenda kule kusaidia tu. Wakati wa
kufanya Site meeting (vikao eneo la mradi). Mimi nilikuwa Arusha
nitakuwaje consultant Kilimanjaro? Watakuwa wamempotosha Waziri,”
alisisitiza Ndossa.
Licha ya kukana, wakati Dk Magufuli akikagua jengo
la ofisi ya mkuu wa Wilaya Siha, alielezwa kuwa, ujenzi wa jengo hilo
uliokuwa chini ya viwango na ulisimamiwa na Ndossa .
Mwakifugile alisema malighafi zilizochanganywa katika ujenzi huo, zilipunguzwa tofauti na viwango vilivyotakiwa.
“Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na vyombo
husika, hii slab ilitakiwa ijengwe milimita 175, badala yake imejengwa
milimita 150, lakini pia hata malighafi haikuwa imefikia kiwango
kinachotakiwa,” alisema.
No comments:
Post a Comment