ADV

ADV

ADVERTISEMENT CORNER

HUDUMA YA KUKATA TICKET ZA NDEGE ONLINE


SOMA HABARI

SOMA HABARI

Wednesday, October 17, 2012

Neno La Leo: Ya Mbagala Na Bedui Aliyekojoa Msikitini...


Ndugu zangu, 

 Moja ya hadithi za Mtume Muhammad S.A. W ni pale Mtume Muhammad alipokuwa msikitini na maswahaba wake. Mara akaingia msikitini mtu wa kabila la Mabedui na kuanza kukojoa. Maswahaba wa Mtume wakasimama kwa hamaki kutaka kumwadhibu Bedui yule. 

Mtume akawasihi maswahaba wake wasifanye jambo lolote litakalomdhuru Bedui yule. Hapo ikavutwa subira. Bedui yule akakojoa na akamaliza. Mtume Muhammad alipomuhoji Bedui yule ikabainika kuwa alikuwa ni mtu wa hovyo na wala hakujua kuwa alimokuwa ni msikitini. Bedui yule akaelimishwa, akaelewa. Akarudi kwenye ustaarabu. 

Ndio mkojo ule ulifutwa kwa maji na amani ikawepo. Wahenga walinena; Subira yavuta heri. Siku zote, hamaki si jambo jema. Kwa kutanguliza subira na kutumia hekima Mtume Muhammad aliivuta heri na kuepusha shari. 

Maana, kama Mtume alisingewaasa maswahaba wake kuvuta subira, basi, makubwa matatu yangetokea ndani ya msikiti ule; Mosi, zingezuka vurugu na watu kuumizana na hata kutoana roho. Pili, mkojo wa Bedui yule ungesambaa msikitini kwa vile alishaanza kukojoa na isingekuwa rahisi kwake kukatisha mkojo wake. Tatu, Mkojo una madhara ya kiafya pia. 

 Naam, kwa mwanadamu, ni muhimu kuwa na subra na kutafakari kabla ya kufanya maamuzi. Kwa ndugu zangu Waislamu, tunaona Mtume Muhammad ameweza kuonyesha hilo. Na kwa ndugu zangu Wakristo, kuna mifano pia ya Yesu Kristo kuonyesha subra. 

Ndio, Uislamu, kama ilivyo kwa Ukristo na dini nyingi za humu duniani, msingi wake ni amani na upendo. Kitendo cha mtoto yule wa Mbagala kukojolea korani kitazamwe kwa sura ya kitendo kilichofanywa na mtoto . 

Na kama ilivyokuwa kwa Bedui yule, kama pale Mbagala subira na hekima vingetangulizwa, basi, yumkini tungebaini kuwa mtoto yule hakujua madhara ya kitendo chake. Naye angekanywa kama tuwakanyavyo watoto wetu. Na hata kitendo hicho kingefanywa na mtu mzima, bado tulikuwa na haja ya kutanguliza subira na hekima kumhoji aliyetenda, yaweza akawa kama Bedui yule kwenye msikiti alimosali Mtume na maswahaba wake. 

Na kwa kuangalia picha zile za Mbagala naiona hatari iliyopo sasa, kuwa tuna vijana wengi wasio na kazi; Wakristo kwa Waislamu. Vijana wasio na dogo. Ni kama moto uliofifia. Akipatikana kwa kuchochea kuni wanalipuka. 

Ni vijana wanaopatikana wakati wowote na mahali popote. Hata jambo likianza saa tatu asubuhi wao wapo. Hawana ofisi wala bosi wa kumwomba ruhusa ya kwenda kuandamana na kurusha mawe. Ndio hawa wanaonekana wamevaa ' Kata kiuno' na wengi wao hawajahi hata kuingia misikitini au makanisani. 

Inakuawaje kijana wa kweli wa Kiislamu achome kanisa na kuiba kompyuta. Inakuawaje kijana na muumini wa kweli wa Kiislamu aonekane saa mchana wa jua kali akivamia baa na kukimbia na kreti za bia? Ni maswali yanayotutaka tutafakari kwa makini. 

Maana, ninavyoamini mimi, uchumi na elimu duni ndio hasa vinavyochochea  vurugu za kijamii, iwe za kidini au kisiasa, na hususan inapohusisha vijana.   Vijana wetu hawana misingi mizuri ya elimu, na wengi hawana ajira pia. Haya ni sawa na makombora yasiyo na gharama kubwa kuweza kutumiwa na wanasiasa wasio waadilifu na hata viongozi wa kidini wenye mitazamo mikali.  Ni makombora yaliyoanza kutulipukia. Tuliziona ishara, tukazipuuzia.

Leo  Kuna vijana watakaotumiwa au kutumia fursa hiyo kutenda maovu kwa kisingizio cha dini. Ni hawa wataoshiriki kuchafua taswira za dini husika pia. Tujiadhari, kabla ya hatari kubwa inayotujia. Hatujachelewa.

 Na hilo ni Neno La Leo. 

Maggid Mjengwa, 

Iringa.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...