Mkurugenzi wa Haki za Binadamu CUF Salim Bimani akifafanua jambo
kupitia Katiba katika mkutano wake wa kupinga matumizi mabaya ya
Operesheni inayofanywa na Jeshi la Polisi na Vikosi vya SMZ kuwatafuta
wavunjifu wa amani.
Baba wa Marehemu Hamad Ali Kaimu ambaye mwanawe alifariki kutokana na
kudaiwa kupigwa vibaya na vikosi vya ulinzi na Usalama akitoa maelezo
kuhusu mauaji ya mwanawe
Waandishi wa vyombo mbali mbali vya habari wakifuatilia kwa makini
taarifa ya Chama cha CUF iliyotolewa na Mkurugenzi wa Haki za Binadamu
CUF Salim Bimani kuhusu kupinga matumizi mabaya ya Operesheni
inayofanywa na Jeshi la Polisi na Vikosi vya SMZ kuwatafuta wavunjifu wa
amani.
Waandishi wa vyombo mbali mbali vya habari wakifuatilia kwa makini
taarifa ya Chama cha CUF iliyotolewa na Mkurugenzi wa Haki za Binadamu
CUF Salim Bimani kuhusu kupinga matumizi mabaya ya Operesheni
inayofanywa na Jeshi la Polisi na Vikosi vya SMZ kuwatafuta wavunjifu wa
amani.Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar
----
MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 29/10/2012
SERIKALI INAUKUZA MGOGORO ULIOPO BADALA YA KUUDHIBITI
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwanza
napenda kuchukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwenu kwa
kukubali wito wa kuja kutusikiliza. Sisi Chama cha Wananchi, CUF,
tunatambua na tunathamini mchango wenu mkubwa na jitihada zenu nyingi,
katika kusaidia kuhamasisha hali ya amani na utulivu ndani ya nchi yetu.
Ni katika kuendeleza hali ya amani na utulivu ndani ya Nchi, suala
lililopelekea kukuiteni leo hapa na kukuelezeni kile ambacho sisi
tunakiona kuhusiana na hali tete inayoendelea hapa Zanzibar, na Tanzania
kwa ujumla.
Ndugu Waandishi,
Naamini
mnatambua kuwa Msingi mmoja, Mkuu wa Chama cha CUF, ni kulinda,
kusimamia na kutetea haki za binadamu pamoja na kuleta amani, umoja,
mapenzi na mshikamano miongoni mwa wananchi wote baada ya kuchoshwa na
hali ya uhasama, chuki, migogoro, mifarakano, mapambano na ugomvi wa
kisiasa uliodumu kwa muda mrefu hapo kabla. Mpasuko wa kisiasa
uliokuwepo, ulisababisha kutokea maafa na mauwaji makubwa ya wananchi na
Wana-CUF, wasiokuwa na hatia, zaidi ya 45 mnamo Jjanuari, mwaka 2001,
yaliyotekelezwa na Jeshi la Polisi la Tanzania na Vikosi vya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, SMZ.
Kupitia
Maridhiano ya Wazanzibari, yaliyoasisiwa na Rais Mstaafu wa awamu ya
Sita ya Uongozi wa Zanzibar, Dr Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa
Chama cha CUF, ambaye pia kwa sasa ni Makamo wa Kwanza wa Raisi wa
Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, November 5, 2009 ndipo Zanzibar Mpya
ya amani, utulivu, umoja na mshikamano ikazaliwa.
Ndugu Waandishi,
Ndiyo
matarajio yetu sote bila shaka kwamba Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, SMZ, pamoja na majukumu yake mengine, inawajibika kuwajali,
kuwathamini, na kuwalinda Wananchi wote, na mali zao, chini ya Misingi
ya Hikma, Haki, Sheria, na Uadilifu. Matumaini hayo ya umma yamekuwa
yakizorota na kutoweka kabisa, usoni mwa kila mwenye hisia za
kibinaadamu na mpenda haki, ndani na nje ya Visiwa vya Unguja na Pemba,
kadiri siku zinavyokwenda, licha ya Nchi kupita katika wimbi la
machafuko, hivi karibuni.
Ndugu Waandishi,
Kiini
na chanzo cha hali hiyo bila shaka kinaeleweka, ambapo kama
ilivyoripotiwa kutoka baadhi ya Mamlaka za Serikali, machafuko hayo,
pamoja na sababu nyengine, yametajwa kutokana na fujo za tarehe 17 na 18
Oktoba, 2012 zlizofanywa na baadhi ya watu au vikundi ambavyo kimantiki
kufanya hivyo ni kwenda nje ya busara na utiifu wa Sheria. Fujo hizo
zimesababisha uharibifu mkubwa wa mali za umma, wananchi mmoja mmoja na
hata vyama vya siasa. Miongoni mwa vitendo hivyo ni kuvunjwa kwa maduka,
vyombo vya usafiri, kukatwa miti ovyo na nguzo za umeme, uharibifu wa
miundombinu zikiwemo barabara, pamoja na kuchomwa moto Maskani za CCM.
Matukio mengine ya kusikitisha na kuhuzunisha zaidi kupitia vurugu hizo
ni kuuwawa kikatili kwa Askari Polisi, Koplo Said Abdulrahman, na watu wasiojulikana pamoja na kuuliwa kwa risasi kijana Salim Hassan Mahoja katika maeneo ya Amani Fresh na watu waliotajwa kuwa wahusika wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Ndugu Waandishi,
Jeshi
la Polisi likishirikiana na Vyombo vyengine vya Ulinzi na Usalama,
vikiwemo Vikosi vya SMZ, limeanzisha oparesheni inayoitwa ya kuwasaka
wahalifu na wafanya fujo za tarehe 17 na 18, Oktoba, mwaka huu. Katika
kile ambacho kinashangaza sana, ni jinsi oparesheni hizo zinavyoendeshwa
na kusimamiwa katika maeneo mbali mbali ya manispaa ya Zanzibar,
hususan katika Mkoa wa Mjini Maghribi. Bila shaka pahala popote duniani
panapohitajika kufanywa Oparesheni za kuwasaka wahalifu wa aina
yoyote, mamlaka husika ndizo zinazobeba dhamana na jukumu la kutumia
utaalamu, mafunzo na mbinu zinazoepusha ukiukaji wa haki na kufanikisha
lengo lililokusudiwa, kwa kufuata Sheria. Hatimaye ni kuwashika wahalifu
na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake
na anaefikishwa katika vyombo hivyo hutakiwa apate fursa ya kusikilizwa.
La
kushangaza zaidi, Jeshi la Polisi upande wa Zanzibar, likishirikiana na
Vikosi vya KMKM, KVZ na JKU wamekuwa wakiliendesha zoezi hilo la
kuwasaka wahalifu kwa uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu, vitisho,
unyanyasaji wa raia na mauwaji. Matukio ya Zanzibar hayana tofauti kubwa
na matukio ya kule Mwanza na Dar es Salaam. Kule Mwanza kamanda wa
polisi wa Mkoa huo Libertus Barlow aliuliwa
kwa kupigwa risasi siku ya tarehe 13, Oktoba 2012 na hatukuona serikali
ikiwaamuru askari wake kufanya uvamizi wa vijiji, uvunjaji majumba,
upigaji kiholela wa watu, maonevu ya wanawake, wizi na uharibifu wa mali
na mauwaji kama inavyofanyika hivi sasa hapa Zanzibar. Kilichofanyika
Mwanza ni msako ulifanyika kitaalamu kwa taratibu za kiupelelezi na
kiasi cha watu watano tayari wamekamatwa kwa lengo la kufikishwa katika
vyombo vya sheria na kuripotiwa katika vyomba vya habari.
Halkadhalika
katika matukio ya Dar es Salaam hivi karibuni, tuliona jeshi la polisi
likishirikiana vyombo vya ulinzi na usalama likitumia mbinu kadhaa
kukabiliana na waandamanaji na kuwakamata watuhumiwa wa fujo hizo.
Hatukuona vitendo vya uvamizi na mateso ya watu wasio na hatia kwa muda
wa siku nne mfululizo kama inavyofanyika hapa Zanzibar. Hatusemi
serikali isiwasake waliofanya fujo na wahalifu waliomuua Coplo Said
Abdulrahman, iwasake na iwafikishe wahusika wote katika vyombo vya
sheria lakini sio watumie kisingizio hicho kufanya hujuma, mateso,
unyanyasaji na muwaji kwa wasio na hatia ambao wengi ni wafuasi wetu wa
CUF.
Ndugu waandishi,
Tokea
tarehe 25 Oktoba 2012 jeshi la polisi na vyombo vyengine vya ulinzi na
usalama kwa hali ya utumiaji mkubwa wa nguvu limekuwa likivamia maeneo
ya Amani, Magogoni, Daraja-bovu, Mwanakwerekwe, Mtoni, Kinuni,
Kwamtipura, Mboriborini, Kilimahewa, Mpendae, Mikunguni, Nyerere,
Kwarara, Tomondo na Nyarugusu ambapo hufanya msako nyumba hadi nyumba,
na barabarani, kuwapiga, kuwatesa, na kuwakamata raia wasiokuwa na hatia
bila ya kujali na kuiheshimu Sikukuu ya Iddi. Majumba yanavunjwa na
waliomo ndani kuvamiwa na kuteswa. Kituo cha ushoni cha kuwaendeleza
mayatima Bububu (JUDAMA) kilivamiwa na watoto wa kike mayatima kupigwa
vibaya. Wengine walipigwa na kuchukuliwa wakiwemo Khalid Shindano na Suleiman Kichwa.
Wengine walikamatwa na kunyolewa ndevu zao hadharani. Pia yuko
aliepigwa hadi kupoteza maisha. Waliokamatwa na kunyolewa ndevu ni
pamoja na Khamis Khatibu na Moh’d Omar wote wa Fuoni.
Ndugu waandishi,
Chama cha CUF kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kijana aitwae Hamadi Ali Kaimu, mwenye
umri wa miaka 22, mkaazi wa Nyerere. Kijana huyu akiwa yuko katika
shughuli za kulisha ng’ombe wake huko kwao Nyerere alivamiwa siku ya
Ijumaa ya tarehe 26/10/2012 siku ya Idi Mosi na vikosi hivyo vya ulinzi
na usalama wakiendeleza zoezi lao la kusaka wahalifu. Kijana Hamadi
alipigwa vibaya sana hadi kupoteza maisha. Baada ya wazee wake kumtafuta
katika vituo mbali mbali vya polisi hawakufanikiwa kumpata ndipo
walipokwenda kumtafuta katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja. Baada ya
kukosa taarifa zake sehemu ya mapokezi lakini walielekezwa wende chumba
cha maiti na ndipo walipogundua kijana wao, Hamad Ali Kaimu ameshafariki
huku mwili wake ukiwa na majeraha sehemu mbali mbali.
Walioathirika na vipigo vya uvamizi huo mpaka siku ya Jumapili ya tarehe 28/10/2012 ni wakiwemo hawa wafuatao:
Baadhi ya waliovamiwa na kupigwa vibaya
JINA | PAHALA ALIPOPIGWA | |
1. | Juma Abdi | Dukani Bububu |
2. | Khamis (Mshona viatu) | Dukani Bububu |
3. | Asma na watoto wake | Ndani ya nyumba yao Bububu |
4. | Juma na mke wake | Dukani Bububu |
5. | Kocha Taibu | Dukani Bububu |
6. | Muuza magazeti | Barabarani kazini kwake Bububu |
7. | Ali Yussuf Choki | Dukani Bububu |
8. | Ubwa na wateja wake | Gareji Bububu |
9. | Shamis Amiri | Dukani Bububu |
10. | Mtoto mdogo wa miaka mitatu (3) wa Bi Salma Faki | Nyumbani kwao Bububu |
11. | Zahor Khalfan | Bububu |
12. | Ahmed | Bububu |
13. | Mashavu Mbarouk | Bububu |
14. | Khalfan Moh’d | Bububu |
15. | Suleiman Ali Alawi | Bububu |
16. | Ali Suleiman | Bububu |
17. | Said Suleiman | Bububu |
18. | Salma Abdalla | Bububu |
19. | Raya Moh’d (Robo) | Bububu |
20 | Ali Abdalla Saleh | Bububu |
21 | Salum Raza | Bububu |
22. | Khalfan Abdalla Ali | Bububu |
22. | Nayadi Moh’d | Kikwajuni |
23. | Miraji | Jang’ombe |
Ndudu waandishi,
Chama
cha Wananchi, CUF kinalaani kwa nguvu zake zote vitendo vya fujo na
uvunjifu wa amani vilivyofanywa siku ya tarehe 17 na 18 Mwezi huu
viliyoambatana na mauwaji ya Coplo Said Abdulrahman, sambamba na hilo
kilanaani kwa nguvu zote na kusikishwa mno na mauwaji, vipigo, uonevu,
unyanyasaji, mateso kwa raia wasio na hatia, kurejeshwa kwa hali ya
chuki, uhasama, kupaliliwa kwa vitendo vya ubaguzi baina ya uunguja na
upemba. CUF inalaani azma ya kuwanyanyasa wananchi na hujuma hizo
zilizopindukia mipaka zinazohamasishwa na baadhi ya Watendaji wa Vikosi
na Vyombo vya Dola, kwa utashi na maslahi binafsi. Tunaamini vitendo
hivi vinatoa fursa pana kwa wale ambao hawautaki umoja wa wazanzibari na
kutoitakia mema Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar.
Ndugu waandishi,
Chama
cha Wananchi, CUF, kinalaani azma na vitendo vyote hivyo vinavyoiweka
haiba ya Nchi katika hali ya machafuko, wakati ambao Wananchi wamekuwa
watulivu licha ya hali tete ya kisiasa. Wazanzibari wengi tayari
wameshapoteza maisha huko nyuma tutokako na wengine kuachwa na ulemavu
wa maisha kupitia hujuma kama hizi zinazofanywa na askari wetu kwa
visingizio hivi na vile. Sisi tunadhani hayo yametutosha na ndio
tukaamua kuingia katika enzi mpya ya Maridhiano, yaani kuishi kwa amani,
utulivu na kuheshimiana. CUF inaamini Vitendo hivyo bila shaka
havitatui mgogoro na tatizo lililojitokeza bali ni uvunjifu wa haki za
binadamu na vinapalilia zaidi hasama na kushawishi mwendelezo wa
uvunjaji wa amani.
Chama
Cha wananchi CUF, kinamtaka Kamishna wa Jeshi la polisi Zanzibar, Bwana
Mussa Ali Mussa kuhakikisha anakomesha vitendo vyote vya unyanyasaji
vinavyofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia wasio na hatia na hapo
hapo kuwachukulia hatua wale wote wanaotenda unyanyasaji huo. Chama cha
wananchi CUF kinamtaka waziri wa nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais,
Mhe Mohammed Aboud Mohammed kuhakikisha serikali inaheshimu haki za raia
wake chini ya misingi ya utawala bora.
Pamoja
nakuiwacha Sheria ichukue mkondo wake, ni vyema Serikali na Vyombo
vyake vya Dola kutekeleza wajibu na majukumu yao kwa
kuzingatia sheria, haki, hikma na uadilifu, bila kuwahujumu na
kuwasumbua Wananchi wasi na hatia, ikieleweka kuwa wao ni sehemu muhimu
ya maisha na raia halali wa Nchi hii.
Naomba kuwasilisha.
HAKI SAWA KWA WOTE
Salim Bimani
No comments:
Post a Comment