Waziri
Kivuli wa Fedha na Uchumi, Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Mbunge
wa Kigoma Kaskazini ndugu Zitto Zuberi Kabwe ameanza ziara ya kikazi
nchini Ujerumani ambapo atahudhuria na kuhutubia Mkutano mkubwa wa
masuala ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Ujerumani na Africa. Mkutano
huo “Economic Conference: Commitment to Africa Initiative” utafanyika
Jijini Berlin kuanzia tarehe 9 – 11 Desemba 2012 na umeandaliwa na
Wizara ya Ushirikiano wa Kimaendeleo ya Serikali ya Ujerumani.
Katika
ufunguzi wa Mkutano huo ndugu Zitto atatoa mada kuhusu mgongano wa
maslahi kati ya Kampuni binafsi na Jamii ambapo ataongelea suala zima la
makampuni makubwa ya kimataifa yanavyonyonya rasilimali za Afrika bila
kuwajibika kulipa kodi na kuendeleza jamii zinazozunguka shughuli zao.
Atazungumzia pia mitaji kiduchu inayokuja Afrika na fedha nyingi
inayotoroshwa Afrika kupitia rushwa, ukwepaji kodi na wizi wa
rasilimali. Afrika inapoteza zaidi ya dola za kimarekani 583 bilioni
kila mwaka kutokana na utoroshaji wa fedha unaofanywa na makampuni ya
kimataifa kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa Afrika. Hata hivyo
Afrika inapokea takribani dola za Kimarekani 80 bilioni tu kwa mwaka
kutokana na Uwekezaji (FDI) na Misaada (foreign Aid). Tanzania ni moja
ya nchi inayopokea misaada mingi kutoka nje na moja ya nchi ambayo
rasilimali zake zinatoroshwa na baadhi ya viongozi wake kutorosha fedha
na kuzihifadhi kwenye mabenki ya Ulaya kama Uswiss.
Mnamo
tarehe 11 Desemba ndugu Zitto atakuwa kwenye jukwaa moja na Waziri wa
Maendeleo wa Ujerumani kuzungumzia namna bora ya kushirikiana kati ya
Ujerumani na nchi za Kiafrika. Miongoni mwa mapendekezo ya Zitto ni
kuondokana na mfumo wa sasa wa ushirikiano wa misaada na badala yake
kuwe na ushirikiano wa kujengeana uwezo ili kila nchi iweze kuhimili
maendeleo yake yenyewe.
Katika
ziara hii Zitto atakutana na Mawaziri Wakuu wa majimbo ya Nord Rhein
Westphalen jimbo ambalo limefanikiwa sana katika vita dhidi ya ukwepaji
kodi unaotokana na raia wa Ujerumani kuficha fedha kwenye mabenki ya
Uswiss na wa jimbo la Lower Saxony kwa ajili ya mazungumzo kuhusu
ukarabati wa Meli ya Liemba na kujenga mahusiano kati ya Mkoa huu na
Mkoa wa Kigoma pia kati ya mji wa PapenBurg na Manispaa ya Kigoma.
Zitto
anatarajiwa kutembelea baadhi ya nchi nyingine za Ulaya na kukutana na
watu mbalimbali katika kuimarisha mtandao wa kimataifa dhidi ya
utoroshaji wa fedha kutoka Afrika (illicit money transfer). Pia
atakutana na watu binafsi wenye ujuzi na weledi katika masuala haya ya
kupambana na watoroshaji wa fedha. Zitto anataraji kurudi nchini mnamo
tarehe 16 Desemba 2012. Kwa namna itaakavyowezekana umma utapewa taarifa
kuhusu ziara hii kupitia akaunti ya twitter na facebook ya ndugu Zitto.
Pia mada zote atakazowasilisha zitawekwa kwenye blogu ya zittokabwe.com kila itakapowezekana.
Waziri
Kivuli wa Fedha na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni anawatakia
Watanzania wote kila la kheri katika Sikukuu ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Utu, Uzalendo, Uadilifu na Uwajibikaji ni silaha muhimu sana za kujenga
Taifa lenye heshima na jamii ya watu wenye fursa za kuendeleza maisha
yao kwa haki na amani. Tutimize wajibu wetu katika kuijenga Tanzania
tuitakayo kwa ajili yetu na kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Imetolewa na Ofisi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
No comments:
Post a Comment