Rais
Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa zamani wa Madagascar Marc Ravalomanana
wakati wa mkutano na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es salaam leo
December 11, 2012.
Na Veronica Kazimoto – MAELEZO
Rais
wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete amefanikiwa
kufanya mazungumzo na Rais wa zamani wa Madagaska Marc Ravalomanana
ambaye amekubali kurudi nchini kwake baada ya kuwa uhamishoni nchini
Afrika Kusini tangu mwaka 2009.
Akizungumza
na wahariri wa vyombo vya habari Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Rais
Kikwete amesema Ravalomanana amekubali pia kutokugombea katika uchanguzi
utakaofanyika nchini humo mwezi Mei 2013 ili kuleta amani na utulivu.
“Nimezungumza
na Rais Ravalomanana na amekubali kurudi nchini kwake madagaska na
kukubali kutokukugombea uchaguzi ujao kama maamuzi ya Jumuiya ya
Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) yalivyofikiwa katika vikao
vyake vya hivi karibuni”, amesisitiza Rais Kikwete.
Raisi
kikwete amefafanua kuwa Ravalomanana anarudi nchini Madagaska bila
masharti yoyote na atapewa ulinzi na Serikali ya nchi hiyo ikisaidiana
na Jumuiya ya SADC.
Kwa
upande wake Rais Ravalomanana amemshukuru Rais kikwete kwa kufanikisha
mazungumzo hayo na amesema anaheshimu maamuzi yaliyotolewa na SADC kwa
lengo la kuisaidia Madagaska kuwa katika hali ya amani.
“Ninamshukuru
Rais Kikwete kwa kufanikisha mazungumzo haya na niko tayari kurudi
nchini kwangu kujenga, kuimarisha na kushirikiana na wananachi ili
kuleta amani na utulivu,” amesema Ravalomanana.
Rais
kikwete alipewa jukumu na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa
Afrika la kufanya mazungumzo na Marais wote wa wawili, Rais wa sasa wa
Madagaska Andry Rajoelina na Rais wa zamani Marc Ravalomanana ambapo
mazungumzo bado yanaendelea kwa upande wa Rais Rajoelina.
No comments:
Post a Comment