Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA,Mh Zitto Kabwe
---
Maandamano ya amani yaliyofanyika mjini Mtwara siku ya alhamis wiki
hii yameibua hoja mbali mbali kutoka kwa viongozi, wananchi, vyombo vya
habari na mjadala wa siku nzima kwenye mitandao ya kijamii hasa
facebook, twitter na JamiiForums. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameita
waandamanaji wapuuzi na Waziri wa Nishati na Madini amewaita watu hatari
na wahaini. CHADEMA tumetoa kauli kupitia kwa Waziri Kivuli wa Nishati
na Madini kwamba udhaifu wa utendaji serikalini ndio chanzo cha
maandamano haya.
Lakini kuna tatizo kubwa zaidi ambalo linaonekana siyo katika sekta
hii tu bali pia katika sekta nyingine ambapo tunaona matokeo yake katika
maisha ya watu wetu na naweza kusema ni dalili za kushindikana kwa sera
za CCM. Sera hizi ndizo ambazo zimelifikisha taifa hili hadi hapa. Kama
hadi wananchi wa Mtwara ambako kwa muda mrefu imekuwa ni ngombe ya CCM
wanaanza kuhoji matokeo ya sera za chama tawala basi ni dalili kuwa
Watanzania wamefungua macho yao na wanaona.
Wanaona katika nishati, wanaona katika utawala bora, wanaona katia
elimu (kuanzia ya msingi hadi ya juu kabisa!), wanaona katika afya,
wanaona katika utendaji wa jeshi la polisi wanaona katika madini. Sera
za CCM zimeshindwa. Zimeshindwa kuinua maisha yao na zinaonekana
kuendelea kushindwa.
Mtwara na Lindi wanataka nini?
Watu wa Mtwara wanataka gesi isiondoke Mtwara na badala yake viwanda
na mitambo ijengwe Mtwara kisha kama ni umeme au mbolea isafirishwe
kupelekwa sehemu nyingine ya nchi. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba Gesi
yote na mazao yake vibaki Mtwara na Lindi. Wanasema umeme uzalishwe
Mtwara usambazwe nchi nzima. Mbolea izalishwe Mtwara na kusambazwa nchi
nzima. Wanataka Bandari ya Mtwara iboreshwe na kuhudumia mikoa ya
Kusini. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba mapato yote ya Gesi yatumike
Mtwara tu la hasha.
Sio dhambi hata kidogo kwa watu wa Mtwara kudai masuala haya. Watu wa
Mtwara wamefanya maandamano kwa amani kabisa bila kuharibu mali na
kutoa maoni yao. Kwanini tuwasute na kuwasusubika kwa madai yao haya?
Kwa nini tusiwasikilize? Kosa lao nini kudai viwanda ili wapate ajira?
Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa masikini kabisa nchini?
Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ilitumika kwa ukombozi wa
kusini mwa Afrika kiasi cha kuwa katika hatari kabisa? Tumesahau
‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara na Lindi dhidi ya usalama wa nchi yetu?
Tumesahau kuwa Korosho imekuwa zao kubwa la biashara na linaloingiza
mapato mengi sana ya Fedha za kigeni? Waziri Muhongo anasema Mtwara
warudishe Fedha za Mkonge na Kahawa. Mbona hataji fedha za Korosho?
Mwaka 2011 Korosho ilikuwa zao la pili kwa kuingiza fedha nyingi za
kigeni baada ya Tumbaku.
Lakini tujiulize, watu wa Mtwara na Lindi walifadi fedha za Mkonge?
Walifaidi fedha za Kahawa? Wamefaidi fedha zao za Korosho? Tumesahau
hata Reli iliyoachwa na Mkoloni ya Nachingwea – Mtwara iling’olewa na
Serikali huru ya Tanzania?
Tujiulize zaidi, hivi watu wa Nzega wamefaidika vipi na Mgodi wa
Resolute pale Lusu? Mgodi umefungwa ukiwa umezalisha na kuuaza dhahabu
ya thamani ya dola za marekani 3.3 bilioni. Hivi katika uhai wa mgodi
huu Serikali Kuu imekusanya kodi kiasi gani? Halmashauri ya Wilaya ya
Nzega imepata ushuru kiasi gani? Watu wa Mtwara wanayaona haya
yaliyotokea Nzega na yanayotokea Tarime, Biharamulo, Kahama na Geita.
Watu wa Mtwara wana Haki kuandamana kuzuia haya yaliyotokea wenzao
yasiwatokee wao kwenye Gesi asilia.
Mtwara na Lindi wanakosea wapi?
Madai yao halali na mimi binafsi na chama changu tunayaunga mkono. Lakini kuna mahala lazima waelimishwe.
Watu wa Mtwara pia wanapaswa kuelewa kuwa juhudi zao zisiwatenganishe
na Watanzania wengine kwani bado utajiri wa Taifa unafadisha kikundi
cha Watanzania wachache sana. Watu wa Mtwara wanahitaji kuungana na watu
wa Mara, watu wa Mwanza, watu wa Shinyanga na watu wa Kagera kudai
utajiri wa nchi utumike kwa maendeleo ya watu badala ya kunufaisha kundi
dogo la watu. Watu wa Mtwara wanapaswa kuunganisha nguvu na Watanzania
wengine kuzuia uporaji wa rasilimali ya nchi dhidi ya kizazi kijacho.
Watu wa Mtwara wasijitenge wakawa peke yao na Gesi yao. Nguvu ya mnyonge
ni umoja.
Serikali isiyosikia
Serikali ina hoja kuhusu kujenga Bomba la Gesi kwa ajili ya kuzalisha
umeme kwa gharama nafuu. Umeme unaotumiwa na asilimia 14 tu ya
Watanzania. Kwa kuwa hii asilimia 14 ndio wenye sauti basi watu wa
Mtwara wataonekana hawana hoja kabisa. Lakini Serikali imejiuliza mara
mbilimbili kuhusu mradi huu wa Bomba? Tunaambiwa na Wataalamu kwamba
kuna uwezekano mkubwa mwakani gesi asilia ya kiasi cha futi za ujazo
trillioni 20 itakuwa imegunduliwa katika Kitalu namba 7( block 7)
ambacho kipo mkoani Dar es Salaam katika Wilaya ya Temeke. Iwapo gesi
nyingi hivi itakuwa hapa Dar karibu kabisa na mitambo ya kuzalisha
umeme, mradi huu wa Bomba unaojengwa kwa trillioni za shilingi utakuwa
na maana tena? Huu mkopo utakuwa na tija?
Serikali imewaambia watu wa Mtwara gharama za kuleta bomba Dar dhidi
ya gharama za kujenga mtambo wa kuzalisha umeme Mtwara na kuusafirisha
umeme kwenda maeneo mengine ya Tanzania? Serikali imeangalia faida ya
kujenga gridi nyingine badala ya kuwa na gridi moja tu yenye kushikwa na
bwawa la Mtera? Leo bwawa la Mtera lisipozalisha hata megawati moja
hata Dar es Salaam izalishe megawati alfu kumi umeme hautakuwapo maana
uti wa mgongo wa gridi ni Mtera! Kwa nini tusiwe na gridi nyingine yenye
uti wa mgongo Lindi au Mtwara?
Tuwasikilize watu wa Mtwara
Watanzania sio mabwege tena. Kuwaita watu wa Mtwara ni wahaini,
wapuuzi au watu hatari haisaidii kujenga Taifa moja lenye watu huru.
Serikali na wadau wote wa sekta ya Gesi likiwemo Bunge washirikiane na
watu wa Mtwara kuhusu miradi ya gesi asilia. Tuwe na Azimio la Mtwara,
tamko la kuelekeza namna bora ya kutumia utajiri wetu wa Gesi bila
kuathiri umoja wa Taifa letu.
Ujio wa Sera, Maono na Uongozi Mbadala
Sasa hivi wananchi wa Mtwara kama wananchi wa sehemu nyingine
wanahitaji maono mbadala, uongozi mbadala, sera mbadala na mwelekeo
mbadala wa kitaifa ambao utaangalia mahitaji yao, utazingatia raslimali
zilizopo na utaunganisha utendaji wa sekta mbalimbali katika kutengeneza
mfumo wa kiutawala na kiuchumi ambao utaliinua taifa zima.
Ni kwa sababu hiyo naamini chama changu ni jibu sahihi kwa matamanio
na kiu ya wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine nchini. Ikumbukwe kuwa
katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya 2010 tulielewa haja ya kuangalia mikoa
hii ya Kusini kwa namna ya pekee na kuipa mwelekeo wa kipekee katika
sera. Bado tuna makusudio hayo tunapoelekea 2015 na tukishika Dola
wananchi wa Mtwara na sehemu nyingine zote zilizoachwa pembezoni mwa
mafanikio wajue kuwa wamepata rafiki na mshirika wa karibu wa
kushirikiana nao kuleta maendeleo.
Siyo katika suala la gesi tu bali katika nishati, maji, elimu,
miundombinu, kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii. Mtwara kama ilivyo mikoa
mingine ina raslimali za kutosha kuweza kuwainua wananchi wake kimaisha,
na zaidi ya yote kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi. Hili ambalo ni kweli
kwa Mtwara ni kweli kwa mikoa mingine kama Kigoma, Manyara, Katavi,
Lindi n.k
No comments:
Post a Comment