Kundi la wananchi waliojawa na gazabu wamevamia kituo cha Polisi Kibiti Wilayani Rufiji na kuleta vurugu kubwa kufuatia raia mmoja kufa kwa kile kilichodaiwa kipigo cha Polisi.
Chanzo chetu cha Habari kutoka Kibiti kimeeleza kuwa kijana aliyefariki kutokana na kipigo hicho ni Hamis Mpondi ambaye mauti yamemfika wakati akipatiwa matibabu Hospitali ya Muhimbili.
Habari zaidi zinapasha kuwa hivi sasa wananchi hao wanateketeza nyumba za Askari Polisi hao zilizopo jirani na kituo hicho, licha ya juhudi za Polisi kuwatawanya kwa mabomu kuendelea kufanyika.
Aidha wananchi hao wameanza kufunga barabara kuu ya Kilwa iendayo Mikoa ya Kusini, Lindi na Mtwara kwa mawe, magogo na kuchoma matairi ikiwa ni umbali wa kama kilometa moja kutoka kituo cha Polisi Kibiti.
Hali inaelezwa kuwa inazidi kuwa tete huku Polisi wa Kibiti wakiendelea na jitihada za kudhibiti hali hiyo kwa kufyatua mabomu hewani kujaribu kutawanya umati huo wa watu.