Askofu wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara
miwili Augustino Shao akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na kuwawa
kwa Padri Mushi huko Ofisini kwake Kanisa la Minara miwili.
--
ASKOFU wa kanisa
katoliki jimbo la Zanzibar,Augostino Shao Alisema matukio ya uhalifu
yanayoendelea kujitokeza nchini hasa kwa waumini na viongozi wa kanisa hilo
hayahusiani na itikadi za kidini bali yanafanywa na watu wachache wasioitakia
mema Zanzibar
Hayo yamesemwa na
Askofu wa kanisa hilo Augustino Shao wakati akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake Kanisa la Minara Miwili Shangani, mjini Zanzibar.
Alisema, kuongezeka kwa
matukio ya uhalifu nchini, kunatokana na kutowajibika kwa watendaji wa vyombo
hivyo, jambo alilosema linatoa nafasi kwa watu wenye dhamira ya kuchafua amani
na utulivu uliopo nchini kutenda uhalifu.
“Matukio ya uhalifu,
ubaguzi na chuki dhidi ya ukristo Zanzibar yanaendelea kushamiri kwani watu
waliopewa dhamana ya kulinda na kusimamia amani na usalama wa wananchi
wanaishia kukemea kwa maneno tu badala ya vitendo.pindi kunapotokea matendo
hayo”, alisema Askofu Shao.
“Siwezi kuhusisha
matukio haya na tofauti za dini ya kikiristo na kiislam bali ni ukosefu wa
umakini kwa watendaji wa vyombo vyenye dhamnana ya kusimamia maisha ya
watu.”Aliendelea kusisitiza Askofu
Hata hivyo, alisema
waumini pamoja na viongozi wa kanisa hilo hapa Zanzibar wanaendelea kuishi kwa
hofu na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Aliongeza kuwa,
uongozi wa kanisa hilo ulifanya juhudi za kuzungumza na watendaji wakuu wa
serikali ya Zanzibar tangu lilipoanza vuguvugu la uchomaji makanisa na kufikia
makubaliano ya kushirikiana katika kudhibiti hali hiyo.
Aliwataka waumini wa
dini ya Kikristo na wananchi kwa ujumla kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki cha
msiba wa Padri Evaristus Mushi.
Naye Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Mjini Magharibi Aziz Mohamed, alisema jeshi hilo linaendelea na
upelelezi ili kuhakikisha wahusika wa tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa
katika vyombo vya sheria.
Aliwataka wananchi
kushirikiana na polisi jamii kutoa taarifa zitakazosaidia jeshi hilo
kukamilisha zoezi hilo kwa haraka zaidi.
“Tangu kuuwawa kwa
Padri Evaristus Mushi juzi Jumapili, tuliitisha kikao cha dharura kwa maafisa
mbalimbali wa Polisi, tukapeana majukumu ili kuhakikisha wahusika wanatiwa
mbaroni”, alieleza kamanda huyo.
Akizungumzia suala la
umiliki wa silaha nchini, alisema kwa mujibu wa sheria za Tanzania hakuna mtu
yeyote anayeruhusiwa kumiliki silaha ya aina yoyote isipokuwa kwa kibali maalum
au taratibu zinazotambulika kisheria
No comments:
Post a Comment