Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein.
---
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed
Shein, amepokea kwa mshtuko mauaji ya Padri Evaristus Mushi na kutoa
pole kwa waumini, ndugu jamaa, marafiki na wananchi wote wa Zanzibar
kufuatia kifo hicho.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud ameeleza
hayo jana, Jumatatu, Februari 18, 2013 na kusisitiza kwamba Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi itawasaka
hadi kuwatia mikononi na hatimaye kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria
wale wote waliohusika na mauaji hayo.
Waziri
Aboud ameyaeleza hayo wakati alipozungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake Vuga, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia mauaji ya Padri
Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar Parokia ya Mtakatifu
ST.Joseph, Shangani.
Hapo
jana Dkt. Shein alikutana na Askofu Augustino Shao wa Kanisa Katoliki,
Jimbo la Zanzibar, huko katika Ikulu Ndogo Migombani, Zanzibar na
kueleza masikitiko yake kutokana na mauaji hayo ya Padri Mushi wa Kanisa
Katoliki la Zanzibar, na kuelezea haja ya kuwepo kwa uvumilivu katika
kipindi hichi cha msiba.
Katika
mazungumzo na waandishi wa habari, Waziri Aboud alisema kuwa Serikali
imejipanga vizuri kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama ili
kuhakikisha kuwa watu wote waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa mara
moja .
“Kutokana
na jiografia ya Zanzibar,Tunaelewa kwamba zipo sehemu katika kisiwa cha
Zanzibar ambazo wahalifu wanaweza kuzitumia, hivyo Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na vyombo husika vitaziba mianya yote ili kupambana na
uhalifu “, alisema Aboud.
Alisema
matendo ya uhalifu yanafanywa katika mazingira ya usiri mkubwa kwa
hivyo ili wahalifu hao wakamatwe wananchi hawana budi kutoa
mashirikiano kwa Jeshi la Polisi pale wanapohitajika.
Akijibu
suali la Mwandishi, Mhe.Aboud alikanusha taarifa zilizozagaa mitaani za
kuwepo silaha nyingi mikononi mwa watu wasiohusika na kuwataka wananchi
kuondoa hofu.
Sambamba
na hayo, Mhe. Aboud amewataka viongozi wa dini mbali mbali pamoja na
waumini wa dini zote hapa Zanzibar kuwa wastamilivu katika kipindi hiki
kigumu cha maombolezi.
Aidha,
Waziri Aboud alisisitiza haja ya kuwepo uvumilivu kwa waumini wa dini
zote ili kuirejesha Zanzibar katika historia yake ya kutokuwa na
migongano ya kidini.
No comments:
Post a Comment