JOPO
la Madaktari wa Chuo wa Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili
(MUHAS), limekamilisha utafiti wa chanjo mpya ya virusi vya Ukimwi,
ambao umethibitisha kuwa chanjo ya DNA -MVA ilikuwa salama na yenye
uwezo wa kufanya mwili utengeneze kinga dhidi ya virusi vya Ukimwi
(VVU).
Utafiti huo ulifanyika nchini kati ya mwaka 2007-2010 na 2008-2012.
Utafiti
wa awali uliofanyika kati ya mwaka 2007 hadi 2010, ambao ulijulikana
kama HIVIS-03, ulihusisha askari 60 polisi na magereza wa jijini Dar es
Salaam, ambao walipewa chanjo hiyo na baadaye kuachwa wakiishi maisha
yao ya kawaida kwa muda wa miaka mitano.
Akizungumza
na Mwananchi Jumapili, Profesa Muhammad Bakari, aliyeongoza jopo la
madaktari waliofanya utafiti huo alisema kuwa umezaa matunda na
kuthibitisha kwamba chanjo ya DNA –MVA waliyopewa askari hao, ilikuwa
salama na yenye uwezo wa kufanya mwili utengeneze kinga dhidi ya virusi
vya Ukimwi (VVU).
“Chanjo
hiyo inaweza kutengeneza vichocheo vya kinga dhidi ya VVU kwa asilimia
100 kwa washiriki waliopatiwa chanjo zote tano. Haya ni matokeo mazuri
sana kupita hata matarajio watafiti, pia ni ya muhimu katika harakati za
kutafuta chanjo dhidi ya VVU,” alisema.
Profesa
Bakari, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mafunzo wa MUHAS, alisema kwamba
hakuna mshiriki aliyekufa, wala kupata athari za moja kwa moja kwa na
kupatiwa chanjo kutokana na tafiti hizo.
Alisema kuwa askari walioshiriki utafiti huo walifanya hivyo kwa hiari yao hadi kukamilisha utafiti huo.
Alibainisha
kwamba jopo la madaktari bado liliendelea na utafiti zaidi, ulioanza
mwaka 2008 hadi 2012, ili kupata chanjo sahihi ya VVU kwa aina ya pili
ya chanjo ijulikanayo kama TAMOVAC-01(Tanzania and Mozambique HIV
Vaccine Program), iliyohusisha pia nchi ya Msumbiji.
“Hatukuishi
hapo, utafiti wa pili (TAMOVAC-01), ulifanyika kati ya mwaka 2008 na
mwaka 2012. Utafiti huu ulijumuisha pia nchi ya Msumbiji.
Profesa Bakari alisema kuwa utafiti nchini Tanzania ulihusisha washiriki 120, kati yao 60 wakiwa ni kutoka jijini Dar es Salaam.
Alibainisha
kwamba kwa mara nyingine washiriki hao walitoka katika Jeshi la Polisi,
Magereza na raia wa kawaida, huku wengine 60 wakiwa raia wa kawaida
kutoka jijini Mbeya.
Mtaalamu huyo alieleza kwamba utafiti huo pia ulionyesha kuwa mchanganyiko wa chanjo ya DNA-MVA ulikuwa salama.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment