Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limesema
matokeo ya kidato cha nne bado hayajakamilika na kuwa habari zilizozagaa wiki
hii kuwa yapo tayari si za kweli.
Hata hivyo Baraza hilo limebainisha kuwa licha ya kutokamilika, matokeo hayo yanakaribia kutoka kwa mujibu wa ratiba za baraza hilo ambapo hutakiwa kutoa matokeo hayo mwezi Februari.
Akizungumza na mwandishi jana, Ofisa Habari na Mawasiliano wa NECTA, John Nchimbi alisema uvumi wa kwamba matokeo hayo yako tayari ulitokana na kuzushwa kupitia mtandao wa kijamii (Facebook).
Alifafanua kwamba habari kuwa matokeo hayo yameanza kutoka kisirisiri kabla hayajatangazwa rasmi na kwamba hatua hiyo inalenga kuyachakachua, siyo taarifa sahihi.
Aliwataka wananchi kuwa makini na uvumi huo kwa vile endapo matokeo hayo yatakuwa tayari yatatangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo na pia kuwekwa kwenye tovuti ya Baraza pamoja na wananchi kuweza kuyapata kupitia simu zao za mkononi.
“Uvumi huu umetokana na mtu asiyejulikana kufungua akaunti ya facebook yenye jina la Baraza na kuanza kuweka taarifa hizo zisizo sahihi. Napenda kuwajulisha wananchi kuwa Baraza letu halina mtandao kama huo hivyo taarifa hizo si sahihi,” alisisitiza.
Nchimbi alibainisha kuwa matokeo hayo si siri hivyo yakiwa tayari Katibu Mtendaji atayatangaza kupitia vyombo vya habari na baadaye yataanza kusambazwa kwa kutumia mtandao.
Aliwataka wananchi kuwa makini ili wasitapeliwe na wanaojifanya kuwa wanaweza kupata matokeo ya mwanafunzi kabla hayajatangazwa rasmi kwa vile suala hilo haliwezekani.
No comments:
Post a Comment