Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu -Chadema, Zitto Kabwe.Picha na Zitto Kabwe(MB)
----
‘Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya
kuchangia hotuba ya Wizara hii ambayo ni muhimu sana na ni moja ya
Wizara ambazo ni andamizi katika uendeshaji wa Serikali yetu kwa sababu
ndiyo Wizara ambayo inasimamia administration of justice. Kwa hiyo, nafurahi sana kuzungumza leo hii.
Mheshimiwa Spika, nina kitabu cha survey ambayo imefanywa na watu wa REPOA lakini ni kazi ya Serikali na kwa sababu ni kazi ya Serikali, kitabu hicho kinaitwaViews of the People 2007. Kitabu
hiki ni sehemu ya shughuli za utekelezaji wa kila mwaka wa Mkakati Wa
Kupunguza Umaskini na Kukuza Uchumi yaani MKUKUTA. Katika kitabu hiki,
inaonyesha kwamba level ya kutoaminiana mistrusts kati ya
Watanzania imefikia 78%, kwa maana ya kwamba katika kila Watanzania 10
ni Watanzania 8 tu ndiyo wanaoaminiana na kuaminika. Kwa hiyo, katika
kila Wabunge 10 ndani ya Bunge hili ni Wabunge 2 tu ambao akisimama
akizungumza unaweza ukaamini maneno yake, hii ni hali mbaya sana katika
taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nimeanza hili kwa sababu ya mjadala ninaouona wa
suala la Mahakama ya Kadhi. Mjadala huu ukiangalia tu mtiririko wa watu
wanavyochangia, umeligawa Bunge kwa misingi ya dini. Wabunge Waislam
wanatoa sababu zao za kwa nini Mahakama ya Kadhi iwepo na Wabunge
Wakristo wanatoa sababu zao kwa nini Mahakama ya Kadhi isiwepo na
inafikia mpaka kutumia lugha ambazo watu wanaotusikiliza huko nje na wao
wanagawanyika.
Mheshimiwa Spika, sasa sisi wengine tumekuta nchi hii ikiwa united, nchi ambayo watu wote tunaishi pamoja na kwa kuangalia level ya
ujana, wengine tunaamini tutaishi muda mrefu zaidi ya wengine, kwa
hiyo, tusingependa kuona taifa linaparaganyika na wengine tusingependa
kuona kwa macho yetu wenyewe na kwa kweli wengine tupo tayari kusimama
kuona kwamba taifa hili haligawanyiki.
Mjadala huu unahitaji tolerance ya
hali ya juu sana kwa sababu ni mjadala wa imani, mnapoanza kujibizana
kwa imani ni kama wengine wanavyosema uvumilivu utaondoka, tunahitaji tolerance ya hali ya juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bahati mbaya sana haujaja Muswada, kuna maelezo,
kwa wale ambao wanasema kwamba Mahakama ya Kadhi iwepo, ni haki yao
kusema kwamba Mahakama ya Kadhi iwepo, tutakuja kukubali au kukataa
tutakapoona kwamba Muswada huu unakidhi haja. Lakini majibizano ambayo
yanaendelea sasa hivi siyohealth hata kidogo kwa sababu akisimama
Mbunge Salum akamjibu Mbunge Paul, Paul na Salum ambao si Wabunge
wataendelea kujibizana huko nje.
Mheshimiwa Spika, mimi nadhani tuwe watulivu na tuwe tolerant, tusikilize
hoja za kila upande kwa sababu hata baadhi ya lugha ambayo inatumika si
nzuri, kwa sababu atasimama mtu atasema wenzetu wanasema hivi,
Mheshimiwa Spika ukisema wenzetu kwa mfano Mheshimiwa Godfrey Zambi
amesimama anasema wenzetu wanasema hivi maana yake ni kwamba tayari kuna
makundi kwamba kuna hawa wenzetu na hawa si wenzetu.
Mheshimiwa Spika, mimi nisingependa tufikie katika hali ya namna hiyo
ningependa mjadala huu uwe mpana zaidi, uwe mjadala wa hoja zaidi,
tusikilizane, tuangalie imani za kila mtu na tuweze kuona na wala sio
kwamba mimi niseme tu kwa sababu limekuwa likizungumzwa, hujibu hoja ya
kwamba ni lazima Mahakama ya Kadhi iwepo kwa kusema ikiwepo na hao
wengine wataanzisha Mahakama yao, inawezekana hao wengine hawana
utaratibu wa aina hiyo. Ndiyo maana ni lazima na ni muhimu sana tuweze
kuhakikisha kwamba mjadala wa namna hii hautugawi bali unakuwa ni
mjadala ambao ni health vinginevyo hali ilivyo sasa tumehama
Bunge la kuwa Bunge la Vyama Vingi tumekuwa Bunge la dini mbili.
Maana
tumezoea mijadala ni Kambi hii ya Upinzani inapingana na Kambi ya Chama
Tawala lakini toka jana naona mjadala ni kambi ya wanaotaka Mahakama ya
Kadhi na kambi ya wasiotaka Mahakama ya Kadhi. Mimi nadhani tusubiri
hiyo report ambayo Waziri ameizungumzia na ijadiliwe kwa mapana
na tusiingie katika lugha ambazo zinaweza zikatufanya kama taifa tuweze
kugawanyika. (Makofi)’
Haya ni baadhi ya maneno niliyoyasema tarehe 14 Agosti 2008 wakati
nachangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria. Bunge lilikuwa
limewaka moto. Wabunge Waislam wakijenga hoja za kiislam kutaka
mahakama ya kadhi na wabunge wakristo wakijenga hoja za kikristo kukataa
mahakama ya Kadhi. Kulikuwa na Umoja wa Wabunge Waislam na Umoja wa
Wabunge wakristo. Wakikaa kwenye vikao na kupanga namna ya kujenga na
kupangua hoja. Hali ilikuwa mbaya sana. Nikawatazama Wabunge wazee
rafiki zangu na kuwaandikia wasimame kuonya hali ile, hawakusimama.
Nikaomba nafasi kusema.
Hali ikatulia na nilipotoka Mzee Kingunge
Ngombale Mwiru akaniita kunishukuru sana. Mzee Malecela alikuwapo
Bungeni lakini akanitumia ujumbe wa kunipongeza kwa maneno yangu yale.
Lakini mpasuko wa nchi kwa misingi ya dini bado ni dhahiri kabisa.
Tumeshudia vitendo vya watu kuchukua sharia mkononi na kufanya mauaji
dhidi ya watu wengine kwa misingi ya dini zao. Leo Mtanzania mwenzetu
Padri Everist Mushi anapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele. Ameuwawa
kwa kupigwa risasi. Kosa lake nini? Kundi la wahuni wachache limetoa
roho ya Mtanzania kwa sababu tu Mtanzania huyu ni Mkristo. Tumeshuhudia
mauaji pia kwa sababu ya ugomvi wa kuchinja.
Eti sisi Watanzania leo tunagombana kwa sababu ya kuchinja.
Bora sisi wengine tunakula majani tu na hivyo magomvi haya ya
kuchinja, ambayo kwa kweli kwa muda mrefu jamii ilijiwekea utaratibu
wake bila kuingiliwa na serikali, hayatusumbui sana. Hata hivyo
yanasumbua jamii zetu na ni suala la ibada kwa baadhi ya Watanzania.
Kugombana kwa sababu ya kuchinja ni dalili tosha kuwa sasa uzi wa
uvumilivu wa kidini uliokuwa umeshika Taifa hili umekatika. Ni kweli
umekatika, wala tusishtuke.
Tatizo kubwa Tanzania ni utamaduni wa kuficha uchafu. Majumbani kwetu
tunafagia na kuweka uchafu chini ya kapeti na kujidai tu wasafi. Namna
hiyo hiyo ndio tunavyoangalia matatizo yetu ya kijamii na hasa kiimani.
Nimesema hapo juu kwenye hotuba yangu hiyo ya mwaka 2008, Watanzania
hatuaminiani kabisa kabisa. Tunadanganyana sana tunapokutana na
tunapoona tatizo cha kwanza tunakimbilia kutafuta ‘jamii gani ya
kulaumu’ na kulaumu kwa ujumla. Waislam kadhaa wanasema eti nchi
inaendeshwa kwa mfumo kristo hivyo kupendelea wakristo. Wakristo kadhaa
wanasema Waislam wanapendelewa na kulindwa na dola. Lakini hawa waislam
na wakristo wanaolalamika hawakai kuoanisha hayo malalamiko yao ili
kupata suluhisho.
Hawataki kwa sababu pakiwa hakuna ‘tension’ watapata
ajenda? Kuna watu wanaishi kwa migogoro tu.
Suala la udini lipo, linakomaa. Badala ya kulitatua kwa kuchukua
hatua kali za kisheria kwa watu wote wanaosambaza jumbe za chuki
tunabaki kulaumulaumu na kuguguna tu. Udini upo na ni kansa inatula
kidogo kidogo. Nitawapa mfano wa udini dhahiri niliyokutana nao kwenye
uchaguzi jimboni kwangu mwaka 2010.
Jimbo langu lina vijiji 33. Kuna vijiji viwili vilikuwa vina mvuto
tofauti kwangu. Kijiji cha Kagunga kilinipokea vizuri sana mwaka 2005,
wakanipa kura nyingi sana (nilishinda kwa tofauti ya kura 600 dhidi ya
mpinzani wangu Helimenshi Mayonga). Kwa kweli niliwapenda watu wa
Kagunga na kufanya kazi nyingi za maendeleo kule ikiwemo kushawishi
miradi mikubwa ya maendeleo kama ujenzi wa bandari, ujenzi wa soko na
hata kupeleka umeme na kujenga barabara kuunganisha kijiji hiki na mji
wa Kigoma. Kijiji hiki kina wakazi wengi ambao ni waumini wa kikristo.
Kijiji cha Bubango kina waislamu wengi. Mwaka 2005 Kijiji hiki wakazi
wake walinikataa kabisa na kuunga mkono mgombea kutoka chama cha CUF
kwamba eti ni chama cha Waislamu. Ilifikia wakati nilikuwa wala siwezi
kufanya mkutano wa kampeni katika kijiji hiki kwa sababu hawakutaka hata
kuniona. Nilishindwa vibaya sana katika kijiji hiki. Kuna vituo vya
kupigia kura nilipata kura 4 kati ya kura 280 zilizopigwa. Katika
kipindi cha miaka 5 ya ubunge wangu, niliwakasirikia watu wa Bubango na
sikwenda kabisa kuwatembelea licha ya kutuma ujumbe wazee kunitaka
radhi. Sasa tazama nini kilitokea mwaka 2010?
Siku moja nikiwa katika kampeni kijijini Bubango, nikaitwa msikitini
na waumini wakaelekezwa wanipe kura kwa sababu mimi ni mwislamu mwenzao.
Sheikh aliyekuwa anatoa mawaidha akasema msijali Zitto hakufanya lolote
lile hapa kijijini lakini mpeni kura tu kwa sababu ni Mwislamu
mwenzetu. Nikaenda kwenye mkutano wa Hadhara nikawaambia wale watu kuwa
sitaki kura zenu kama mnanipa kwa sababu ya uislamu wangu. Nikaondoka.
Nilishinda katika kijiji hiki. Nilipewa kura kwa sababu ya uislam wangu.
Ngome yangu ya kampeni ilikuwa Kagunga. Ndipo nilipoweka nguvu zangu
maana ninapendwa na nilifanya mambo makubwa. Siku chache kabla ya
kampeni, ilikuwa siku ya jumanne nikaitwa kwenda Kagunga kwamba mambo
yameharibika sana. Nikataharuki na kupanda boti la kukodi na kwenda
Kagunga nikafika saa nne usiku. Wenyeji wangu wakaniambia kuwa
wametangaziwa kanisani kwamba Zitto asipewe kura kwa sababu akienda
Bungeni ataleta mahakama ya kadhi. Nikaomba kuongea na viongozi wa dini
kesho yake asubuhi, wakaja wachungaji 11 (Kagunga kuna makanisa mengi
sana).
Nikawauliza ni kweli kwamba mimi nisipewe kura kwa sababu ya
uislamu wangu? Wakasema hayo ndio maagizo na wameshawaambia waumini.
Nikawauliza mnaamini katika hayo? Wachungaji wanne wakasema, mheshimiwa
mbunge sisi tupo na wewe. Nikapiga ngoma kuitisha mkutano wa hadhara saa
nne asubuhi pale ziwani Kagunga. Nikawaambia watu wa Kagunga, anayetaka
kuninyima kura kwa sababu ya uislamu wangu aendelee na uamuzi wake.
Nikaorodhesha nini tumefanya Kagunga. Nikasema kama hayo hayatoshi
kuwafanya kuchagua mbunge, basi amueni kwa kutumia imani za dini yenu.
Nikashuka, nikapanda boti na kuondoka. Matokeo yalipotoka, Kagunga
nilishinda kwa tofauti ya kura tisini tu (kutoka kura 600 mwaka 2005).
Toka matukio haya mawili nikasema moyoni mwangu hatuna nchi tena.
Viongozi wamekuwa wakitoa kauli za kugawa wananchi. Kiongozi wa CCM kwa
mfano anaposema CUF ni chama cha Waislam, anawaambiwa waislam nendeni
huko ndio chama chenu. Kiongozi wa CCM anaposema CHADEMA ni chama cha
kikristo, anawaambia wakristo nendeni huko ndio chama chenu. Mwanachama
wa CHADEMA anapotoa taarifa kuonyesha kuwa CCM inapendelea waislamu,
anadhihirisha kuwa kweli chama chake hakipendi waislamu. Viongozi wa
kisiasa wanatoa kauli majukwaani bila kuzipima na kugawa wananchi.
Baadhi ya taasisi za kidini zimekuwa zikutumiwa na vyama vya siasa
kusambaza chuki hizi kwenye jamii.
Mimi ni Mtanzania. Taifa ambalo limejengwa kwenye misingi ya usawa na
haki. Misingi ya Umoja na mshikamano. Tunu zetu ni hizo na sio dini
zetu. Viongozi wanapoendelea kulea upuuzi huu wa udini Taifa litapasuka
vipande vipande. Kwenye masuala ya udini watu hawaweki akili,
wanaongozwa na imani. Mijadala inayoendelea sasa inatugawa sana. Lazima
tukatae. Tuseme udini sio tunu ya Taifa letu, inaweza kuwa tunu ya mtu
binafsi lakini Utanzania wangu ni utu, umoja, uzalendo, uwajibikaji na
uadilifu.
Mtu yeyote yule anayepanda mbegu za udini asionewe aibu.
Ashughulikiwe haraka sana. Wapuuzi Fulani wanasema kwa kuwa Mkuu wa
Polisi ni wa dini Fulani basi ndio maana hachukui hatua. Huyu sio Mkuu
wa polisi wa kwanza nchini wa dini hiyo, kuna aliyekuwepo na akaingiza
msikitini askari polisi na viatu. Tusiruhusu kabisa upuuzi huu kwamba
watu wenye dini Fulani hawachukui hatua dhidi ya watu wa dini zao.
Vyombo vya usalama vijue, mtu anayeua ni muuaji tu na lazima achukuliwe
hatua kwa uuaji wake. Tena uuaji mbaya unaojenga chuki kwa nchi yetu.
Mtu anayetamka maneno ya chuki dhidi ya dini nyingine achukuliwe hatua
bila kujali hadhi yake.
Mwisho hatuna namna, ni lazima Taifa liongee. Lazima tuwe na mjadala
wa wazi na wa kuheshimiana kuhusu masuala ya udini na kuvumiliana
kidini. Hatuwezi kuweka rehani amani ya nchi yetu kwa suala la kuswali
au kusali. Badala ya kurushiana lawama, tuzungumze kwa uwazi. Makundi ya
wananchi wenye kuona uonevu wa kidini waje waseme kwa uwazi na masuala
hayo kujadiliwa kwa uwazi. Muhimu tupate mwafaka na kujenga Taifa imara
na lenye mshikamano.
Kwa nchi yenye utajiri wa rasilimali kama yetu udini ni kichocheo
tosha cha vita ya wenyewe kwa wenyewe na migogoro isiyokwisha. Ni lazima
tuchukue hatua sasa. Tuache unafiki wa kunyoosheana kidole. Kila mtu
atazame nafsi yake na aseme ukweli wake kwa uwazi kabisa. Tusifukie
uchafu chini ya kapeti.
Zitto Kabwe(MB)
No comments:
Post a Comment