Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Bole jijini Addis Ababa, Ethiopia, leo Februari 23, 2013 kuhudhuria
utiwaji saini Mpango wa
Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC).Picha na IKULU
--
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili Addis Ababa, Ethiopia, leo Februari
23, 2013 kuhudhuria utiwaji saini Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Amani,
Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mpango huo unatarajiwa kutiwa saini kesho Februari
24, 2013 na Wakuu wa Nchi kutoka Ukanda wa Maziwa Makuu, ikiwa ni pamoja
na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Uganda, Jamhuri
ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Angola, Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya
Kongo (Brazaville), Jamhuri ya Zambia, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
pamoja na Jamhuri ya Afrika Kusini.
Aidha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Ban Ki
Moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa, Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma,
pamoja na wenyeviti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)
na Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) watatia saini Mpango huo kama mashahidi
na wadhamini.
Mpango huo una nia ya kuchangia juhudi ambazo zimefanywa
na Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika (SADC) katika kutafuta amani Mashariki ya Kongo na ukanda
wote wa Maziwa Makuu kwa ujumla.
Mpango huo pia umetilia maanani
mapendekezo muhimu yaliyokubalika baada ya mashauriano kati ya wakuu
wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) na Jumuiya
ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa.
“Mwisho”
Imetolewa
na:
Muhidin Issa Michuzi,
Mwandishi wa Habari wa Rais,
Msaidizi,
No comments:
Post a Comment