Bwana Yesu alipotembelea mto Galilaya, aliwakuta wavuvi wakivua samaki,
Simoni alikuwa ni miongoni mwa wavuvi hao. Yesu akasema; " Simoni, acha
kuvua samaki,nifuate ukawe mvuvi wa watu.
Naam, watu wengi wanaangamia kwa kukosa uelewa. Kwa kutojitambua.
Wanahitaji ukombozi wa kifikra. Na siku zote, haki uinua taifa, vivyo
hivyo, dhulma huangamiza taifa. Na mahala pasipo na haki, basi, hapo
hapatukuwa na amani.
Oneni, maovu yametamalaki katika dunia tunamoishi. Siku zote, kujipendelea ndilo shina la maovu. Si tuna mifano hai.
Oneni, wale wenzetu waliokaa na wakaamua kuuza nyumba za Serikali. Na
Waziri mwenye dhamana alisimamia utekelezaji wa dhulma ile kwa
Watanzania, huku naye akiwa ameshajikwapulia nyumba yake. Lililopelekea
uamuzi wa hila na ghilba wa kuuza nyumba za serikali ni ubinafsi na
hulka ya baadhi ya viongozi kutaka kujipendelea.
Karibu
wote waliouziwa au kujiuzia nyumba hizo za Serikali, nyumba za
wananchi, tayari walikuwa na nyumba kabla. Siku zote, hamu inakuwa ni
jambo jema, endapo binadamu ataweza kuitawala hamu/tamaa yake.Wanadamu
tusipoitawala hamu yetu, tukaanza kujipendelea, kuwasahau wengine, basi,
hilo huwa ndio chimbuko la maovu.
Hupelekea kutoelewana baina ya wanandugu, na hata kwa marafiki
walioshibana. Hupelekea vurugu na machafuko katika jamii. Tunazungumzia
uwepo wa upendo, haki na usawa.
Dini nyingi zinazungumzia umuhimu wa upendo, haki na usawa katika jamii. Iwe ni Uislamu na Ukristo vivyo hivyo.
”
Naapa kwa zama . Hakika binadamu wote wamo katika hasara isipokuwa wale
walioamini na wakafanya matendo mema. Wakahusiana na haki na
wakahusiana na subira” (Koran tukufu, Surat ASWR) Biblia nayo inasema;
kuwa Kaini alikuwa mtu wa kujipendelea mno, akamwua nduguye. Mfalme
Saulo alijipendelea mno, akamdhulumu Daudi. Yuda alijipendelea mno,
akakubali kumsaliti Yesu kwa Vipande thelathini vya fedha. Hatimaye,
akamsaliti Yesu.
Na
ufufuko wa Bwana Yesu utukumbushe jukumu letu la kupambana na maovu
katika jamii. Utukumbushe jukumu la kusaidia kazi ya kuwakomboa kifikra
wanadamu wenzetu.
Kama Bwana Yesu alivyomkumbusha Simoni kwa kumwambia; ” Simoni, acha kuvua samaki. E nenda ukawe mvuvi wa watu.
Ni Neno la Leo.
Pasaka Njema.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam
0788 111 765
No comments:
Post a Comment