ADV

ADV

ADVERTISEMENT CORNER

HUDUMA YA KUKATA TICKET ZA NDEGE ONLINE


SOMA HABARI

SOMA HABARI

Tuesday, April 23, 2013

Watesaji wa Kibanda, Ulimboka kitendawili: Lwakatare, Ludovick jalada lao lakabidhiwa kwa DPP


Said Mwema IGP

WATEKAJI na watesaji wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk. Stephen Ulimboka, na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, wanaendelea kuwa kitendawili baada ya Jeshi la Polisi kudai linaendelea na uchunguzi.

Wakata jeshi hilo likishindwa kuwatia mbaroni watesaji wa wanataaluma hao, limetamba kukamilisha uchunguzi wake kuhusu kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mungulu, kwa waandishi wa habari jana, jalada hilo limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa hatua zaidi.

Licha ya matukio ya Ulimboka na Kibanda kutokea muda mrefu ikilinganishwa na lile la Lwakatare, Mungulu alishindwa kujibu maswali ya waandishi kuhusu suala ambalo linaonekana kupigwa danadana.

Dk. Ulimboka alitekwa na kuteswa vibaya kwa kuumizwa sehemu mbalimbali za mwili na kung’olewa meno, kucha kisha kutelekezwa katika Msitu wa Mabwepande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, usiku wa kuamkia Juni 26, 2012.

Katika tukio linalofanana na hilo, Kibanda naye alivamiwa wakati akiingia nyumbani kwake na kupigwa kwa nondo kichwani, kutobolewa jicho la kushoto, kung’olewa kucha, meno mawili na kukatwa kidole.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na makao makuu limeunda timu za wataalamu kuchunguza matukio hayo lakini hadi leo zimekuwa zikipigwa danadana ya kuwakamata wahusika.

Katika mkutano wake na wanahabari, Mungulu aligusia matukio hayo kwa kifupi akisema uchunguzi bado unaendelea.

“Kuhusu kuvamiwa, kuteswa, kupigwa na kujeruhiwa kwa Mhariri Mtendaji wa New Habari 2006, Kibanda, tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa Dk. Ulimboka, matukio yaliyotokea Zanzibar, uchunguzi bado unaendelea na uko katika hatua mbalimbali ambazo kwa sasa hakuna umuhimu wa kuziweka wazi kuepusha kuharibu upelelezi,” alisema.

Alipoulizwa ni kwa nini hawajamkamata mtuhumiwa mwingine zaidi ya yule aliyejisalimisha katika kitubio kanisani, Joshua Mulundi, Mungulu alikwepa akiwataka waandishi wasome nakala ya tamko la jeshi hilo.

Hata hivyo nakala hiyo iliyogawiwa haikusema chochote kuhusu tume hiyo kupata watuhumiwa wengine kwa kesi ya Dk.Ulimboka.

Tukio la Ulimboka ni kama jeshi la polisi limeinua mikono kwani Inspekta Mkuu wa Polisi (IGP), Said Mwema, aliwahi kusema mbele ya wakuu wenzake wa mataifa mbalimbali kuwa ni siri ya taifa.

Dk. Ulimboka mwenyewe baada ya matibabu yake nje ya nchi, hajawahi kuhojiwa na jeshi la polisi licha ya kukaririwa na vyombo vya habari akimtaja mtumishi moja aliyedai ni wa Ikulu akidai alihusika kumteka na kumtesa.

Wakati huo huo, Mungulu alisema kuwa upelelezi wa kumwagiwa tindikali kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mussa Tesha, katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga mkoani Tabora September 2011, upo katika hatua za mwisho.
Alisema ingawa watuhumiwa wawili tayari wamefikishwa mahakamani, endapo watapatikana wengine zaidi nao watafikishwa huko

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...