Mbunge wa
Monduli, Edward Lowassa, amesema Baraza la Mawaziri, lilimpinga
asisafirishe maji kutoka Ziwa Victoria hadi wilayani Kahama, Mkoa wa
Shinyanga. Amesema kwamba, siku aliyowasilisha wazo hilo katika baraza
hilo, mawaziri wote walimpinga, isipokuwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na
Mohamed Seif Khatib.(hd)
Lowassa
alitoboa siri hiyo jana, alipokuwa akizungumza katika harambee ya
uchangiaji wa Shule ya Msingi ya Kanisa la AICT, Kahama, Shiyanga.
Pamoja na
hayo, alisema anayetakiwa kupongezwa katika mradi huo ni pamoja na Rais
mstaafu, Benjamin Mkapa, kwa kuwa alishiriki kuufanikisha.
"Niwapeni
siri moja, nilipendekeza waraka wa kutumia maji ya Ziwa Victoria kwa
Rais Mkapa, naye akaniuliza, wale wakubwa tutawaweza? Nikamwambia
tutawaweza, akauleta katika Baraza la Mawaziri.
"Kule
mawaziri wote waliupinga, kasoro Rais Kikwete, ambaye wakati ule alikuwa
Waziri wa Mambo ya Nje pamoja na rafiki yangu, Mohamed Seif Khatibu.
"Mzee
Mkapa baada ya kusikiliza mawazo yote, akaamua fedha zitolewe, na sasa
mnafaidi maji safi kutoka Ziwa Victoria," alisema Lowassa.
Ufafanuzi
huo aliutoa baada ya Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, Khamis
Mgeja, kumsifu Lowassa kwa kuleta maji mkoani humo, ambapo alisema
wananchi wa Shinyanga wanayaita maji hayo kwa jina la Malowassa, yaani
maji ya Lowassa.
Pamoja na
hayo, wakati msafara wa Lowassa unaingia wilayani Kahama, wananchi
walijaa barabarani na kumshangilia, huku baadhi wakionyesha maji kama
ishara ya kutambua mchango wake katika maji hayo.
Lowassa,
ambaye wakati maji yanapelekwa Shinyanga alikuwa Waziri wa Maji na
Mifugo, alisema wakati alipokuwa katika juhudi za kupinga mkataba wa
zamani wa kimataifa unaoipa Misri haki miliki ya maji ya Mto Nile
unaoanzia Ziwa Victoria, alikwenda kwenye mkutano wa maji mjini Cairo,
ambako alikutana na mambo mawili makubwa.
"Wakati
nateremka pale airport, nilikuta ulinzi wa hali ya juu sana, nikauliza
iweje mimi waziri tu nipewe ulinzi namna hii! Mwenyeji wangu akatabasamu
tu.
"Siku ya
pili yake, nikaenda kwenye mkutano na waandishi wa habari, sijawahi
kukutana na idadi kubwa namna ile ya waandishi wa habari, wakati ule wao
walikuwa wanamjua Mwalimu Nyerere na timu ya Simba tu ambayo
iliwafunga, sasa walitaka kumjua huyo Lowassa ni nani mwenye jeuri na
nguvu ya kutaka kutumia maji haya.
"Wakaniuliza,
kwa nini nataka kutumia maji yale wakati kuna mkataba unaozuia,
nikawaambia, kule Tanzania kuna watu wanakaa umbali wa kilomita tano tu
kutoka ziwani, lakini hasa kina mama wanalazimika kutembea umbali mrefu
wa zaidi ya kilomita 20 kwenda kutafuta maji.
"Baadaye
nikawaambia, tutayachota maji yale, mtake msitake, wakashangaa,
nikaondoka na sasa mnaona faida ya msimamo wangu," alisema.
Awali,
Mgeja aliwapiga vijembe wanasiasa wanaompiga vijembe Lowassa, kwa kusema
kuna kikundi cha wanasiasa wahuni wanaomuonea wivu Lowassa.
"Kundi
hili lishindwe na lilegee kwa jina la Yesu," alisema Mgeja, huku
akishangiliwa na waumini, ambapo alimfananisha Lowassa na mto mkubwa
Kkama Ruvu na kwamba hakuna anayeweza kukinga mikono kuzuia kasi ya maji
yake.
Katika
harambee hiyo, Lowassa alichangisha zaidi ya Sh milioni 220, zikiwamo
ahadi na fedha taslimu, japokuwa malengo yalikuwa ni kupata Sh milioni
150. Chanzo mtanzania
No comments:
Post a Comment