Museveni kuwakutanisha Rais Kikwete na Kagame 
                                           
            
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni 
ameitisha mkutano wa dharura wa marais wa nchi za Maziwa Makuu (ICGLR), 
kujadili hali ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya 
Kongo.Rais Jakaya Kikwete ni miongoni mwa waalikwa kwenye mkutano huo 
ambao pia unatarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
         
            
Wakati hali ya usalama Mashariki mwa 
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikidhoofika, katika siku za karibuni, 
uhusiano wa Tanzania na Rwanda umekuwa wa shaka hasa baada ya Rais 
Kikwete kuishauri Serikali ya Rwanda kukaa na wapinzani ili kumaliza 
mzozo uliolikumba eneo la Maziwa Makuu.
Rais Kikwete alitoa ushauri huo wakati
 akiwa katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika 
(AU), zilizofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia. Mkutano wa leo 
utafanyika kwenye Ukumbi wa Commonwealth Resort, Munyonyo katikati ya 
Jiji la Kampala.
Kwa mujibu wa taarifa Rais Museveni 
ameitisha mkutano huo hasa kuzungumzia hatua ya Umoja wa Mataifa 
kupambana na Kundi la Waasi wa M23.
Mbali na viongozi hao wa Tanzania na 
Rwanda, viongozi wengine wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo wanatoka 
Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya
 Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Sudan, na Zambia.
 
 
 
          
      
 
  
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment