ADV

ADV

ADVERTISEMENT CORNER

HUDUMA YA KUKATA TICKET ZA NDEGE ONLINE


SOMA HABARI

SOMA HABARI

Monday, October 7, 2013

ccm chapokea ugeni mkubwa

Chama Cha Mapinduzi Logo 589ae
Leo Jumatatu tarehe 07/10/2013 Chama cha Mapinduzi kinapokea ugeni mkubwa wa Makatibu Wakuu wa Vyama vya Ukombozi Kusini mwa Afrika. Makatibu Wakuu hawa wanakuja kuhudhuria Mkutano wa Sita ambao ni mwendelezo wa mikutano ya aina hii inayofanyika mara mbili kwa mwaka. (hd)
Vyama vyote vya Ukombozi vitahudhuria Mkutano huu utakaofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 09 Oktoba. Vyama hivyo ni ANC cha Afrika ya Kusini; FRELIMO cha Msumbiji, MPLA cha Angola; SWAPO cha Namibia; ZANU-PF cha Zimbabwe na Chama mwenyeji CCM.
Mkutano wa Makatibu Wakuu utatanguliwa na mikutano ya Jumuiya za Vijana, Wanawake na Maveterani itakayofanyika Jumanne Oktoba 8, 2013.
Mkutano wa Sita wa Makatibu Wakuu utahudhuriwa pia na ujumbe kutoka Chama rafiki cha Kikomunisti cha China utakaoongozwa na Ndugu Ai Ping, ambaye ni Naibu Waziri anayeshughulikia Idara ya Kimataifa ya Chama hicho.
Pamoja na mambo mengine Mkutano huu wa Sita wa Makatibu Wakuu wa vyama vya Ukombozi kusini mwa Afrika utajadili utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa katika kikao chao cha tano kilichofanyika huko Tshwane, Afrika ya Kusini mwezi Machi, 2013.
Mojawapo ya maazimio hayo ni ujenzi wa Chuo cha Pamoja cha Vyama hivi vya Ukombozi utakaofanyika Ihemi, katika mkoa wa Iringa. Makatibu Wakuu wanatarajiwa kuzuru eneo la Ihemi tarehe 08/10/2013 kama sehemu ya maandalizi ya majadiliano ya Mkutano huo wa Sita.
Mkutano huu utafunguliwa rasmi na Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi tarehe 09/10/2013.
Imetolewa na :-
Asha-Rose Migiro
KATIBU WA SIASA NA UHUSIANO WA KIMATAIFA
CHAMA CHA MAPINDUZI

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...