London, England. Milango ipo wazi kwa
klabu kubwa za Ligi Kuu England kumsajili kiungo wa Bayern Munich, Toni
Kroos ambaye mazungumzo ya mkataba wake mpya na klabu yake yamevunjika.
Kroos, amekuwa akifuatiliwa kwa karibu na Manchester United hasa wakati wa dirisha dogo la usajili ambalo lilifungwa Januari 31.
Kiungo huyo ambaye thamani yake ni
Pauni 25 aliingia matatani wiki iliyopita baada ya kutolewa katika
mchezo wa Ligi Kuu ya Ujerumani dhidi ya Stuttgart, jambo ambalo
lilimchukiza.
Kitendo hicho kilimchefua kocha wake, Pep Guardiola ambaye ameamua kumwondoa katika kikosi chake.
Uamuzi huo unaungwa mkono na
wakurugenzi wa Bayern ambao pia wamekataa kumwongezea mshahara Kroos
kutoka Pauni 60,000 kwa wiki hadi kufikia Pauni 150,000.
Kroos, anataka alipwe mshahara mkubwa
kama ilivyo kwa nyota wengine, Philipp Lahm, Bastian Schweinsteiger,
Franck Ribery ambao wanalipwa Pauni 150,000 kwa wiki.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 24
amekuwa akieleza kutoridhishwa kwake na mwenendo na vitendo
anavyofanyiwa kwenye klabu hiyo ya Allianz Arena.
Gazeti la Sportsmail wiki iliyopita
liliripoti kuwa kocha wa Man United, David Moyes amekuwa akifuatilia kwa
karibu hali ya kiungo huyo na hata kuwasiliana wakala wake.
Hata hivyo, Man United huenda
ikakutana na upinzani mkali kutoka Man City, Chelsea, Arsenal na
Liverpool, zote ambazo zimeelekeza macho yao kwa kijana huyo. Chanzo:
mwananchi
No comments:
Post a Comment