Rais
Jakaya Kikwete amemwagia sifa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
hatua ambayo inaweza kutafsiri mengi katika medani ya siasa nchini.
Akizungumza
na wabunge wa CCM kwenye Ukumbi wa White House Dodoma juzi, Rais
Kikwete ambaye pia mwenyekiti wa chama hicho,alisema nguvu za Lowassa
pekee zinatosha kushinda uchaguzi mdogo wa kiti cha udiwani Kata ya
Makuyuni kilichoko wilayani Monduli.
Kata ya Makuyuni iko wilayani Monduli, ambako Lowassa amekuwa mbunge wake tangu mwaka 1995.
Habari
za kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa Rais Kikwete alitoa kauli
hiyo kuhusu kampeni za uchaguzi huo wa Makuyuni, baada ya kuwa ametoa
ruksa kwa makada wa chama hicho wanaotaka urais kuanza kujipitisha
pitisha miongoni mwa wanachama wa chama hicho.
Lowassa anatajwa kuwa miongoni mwa wanaCCM wanaotaka kumrithi Rais Kikwete kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
“Sina tatizo na pale Makuyuni, najua muscles (misuli) za Mzee Lowassa zinatosha kutupa ushindi; au vipi mzee?”alidokeza mmoja wa wabunge wa CCM akimnukuu Rais Kikwete.
Uchaguzi
wa Udiwani Kata ya Makuyuni unaotarajiwa kufanyika Juni 16, mwaka huu,
utakuwa wa ushindani mkali kati ya CCM na Chadema ambao historia yao
kisiasa mkoani Arusha ni ya uhasama.
Katika
uchaguzi huo, unaofanyika baada ya kifo cha Abdillah Warsama (CCM),
chama hicho kitatetea nafasi yake kwa kumsimamisha Godluck Lerunya na
Chadema ni Japhet Sironga.
Mbali
na Kata ya Makuyuni, uchaguzi wa udiwani mkoani Arusha utafanyika pia
katika Kata za Kaloleni, Themi, Kimandolu na Elerai, kutokana na
waliokuwa madiwani wa kata hizo (Chadema), kufukuzwa na chama chao.
“Mnaweza
kuchafuana leo, kesho mkapata mgombea mwenye nundu nyingi na mabandeji
kila mahala, halafu mkapata shida kumnadi,” alisema.
Siyo mara ya kwanza kwa Kikwete kumsifia Lowassa kwani aliwahi kufanya hivyo mwaka jana huko Longido wakati akikabidhi ng’ombe.
Pia
aliwahi kumsifia wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2010 wakati
Kikwete alipomwelezea Lowassa kama Mbunge makini na kuwaomba watu wa
Monduli kumchagua tena.
Hata
hivyo, alipoulizwa kama baada ya kuruhusiwa kuanza kujipitisha kwa
wanaCCM kama anataka kuwania urais, Lowassa alijibu kupitia watu wake wa
karibuni kuwa asingependa kuzungumzia suala hilo hasa baada ya Rais
kutoa kauli hiyo.
Kutangaza nia ruksa
Rais
Kikwete aliwaeleza wabunge hao kuwa si kosa kwa watu kutangaza nia ya
kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ikiwamo urais mwaka 2015.
“Wabunge
na mawaziri wenye nia ya kutangaza nia ya kugombea urais wawe huru,
kwani hiyo ni haki yao, isipokuwa wafanye kwa wema bila kukivuruga chama
na kuwagawa wanaCCM katika makundi. Sioni tatizo watu kujipitisha. Sisi
sote hapa tulijipitisha. Lakini tufanye hivyo kistaarabu bila
kuvurugana.”'
Aliwaagiza wabunge wa chama hicho kwenda majimboni mwao kusikiliza kero za wananchi badala ya kusubiri wakati wa uchaguzi.
Kauli ya Membe
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye naye anatajwa kuwa miongoni mwa wagombeaamewataka waandishi waache kuandika kila siku habari za urais na badala yake waandike mambo ya maendeleo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana baada ya kukutana na mabalozi wa nchi
zinazoendelea kuhusu Mkutano wa Smart Partnership, unaotarajiwa
kufanyika nchini, Membe alisema ni vizuri yakaandikwa mambo ya maendeleo
na si kila wakati kuandika mambo ya urais.
“Mkutano kama huu nchi kama Kenya watauripoti vizuri na kwa undani hivyo mfanye hivyo si kila kitu urais 2015,”alisema Membe.
Mkutano huo utaanza Mei 28, hadi Juni Mosi na utajadili jinsi gani sayansi na teknolojia vinaweza kutumika kuzikwamua kiuchumi.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment