
Nguvu ya
makundi ya watu wanaotajwa kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi
(CCM) zinaendelea kukitikisa chama hicho huku makada wake wakitoa
angalizo wakiutaka uongozi wa juu wa kuchukua hatua haraka za kinidhamu
kwa wahusika.
Wiki iliyopita wanachama wa chama
hicho wanaodaiwa kutoka katika kambi tofauti zinazoisaka nafasi ya urais
waliibuka na kutoa kauli zinazoonekana wazi kupigana vijembe, kila
upande ukiuponda mwingine kuwa unavunja kanuni na katiba ya chama hicho.
Malumbano hayo ya makada wa CCM
yanayoonekana dhahiri kuchagizwa na makundi pamoja na wafuasi wa vigogo
wanaousaka urais kupitia chama hicho.
Ingawa makundi yanayosaka urais
kupitia chama hicho ni mengi, ni kundi moja tu linalomuunga mkono
aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa ndilo linaloonekana dhahiri
kupigiwa kelele kwa kutajwa kwa majina bila kificho, hasa baada ya kauli
yake kuwa ameanza safari, aliyoitoa mbele ya wageni wakati wa
kuadhimisha mwaka mpya 2014.
Kutokana na kauli hiyo na mambo
mengine, Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa UV-CCM, Paul Makonda
aliibuka na kumshambulia Lowassa, suala ambalo limeyaibua makundi
mengine, baadhi yakiunga mkono kauli ya Makonda na mengine yakiibeza na
kumshushia tuhuma za kuvunja kanuni za chama.
Mmoja kati ya waliojitokeza ni Makamu
Mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Malecela ambaye ameonyesha waziwazi
kutofautiana na mipango na mikakati ya Lowassa.
Malecela anamuunga mkono Makonda, kwa
kauli yake, ikiwamo kwamba Lowassa anafadhili mikakati ya kupingana na
juhudi za sekretarieti ya CCM chini ya Katibu Mkuu, Abdulrahaman Kinana
na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Wakati Makonda na Mzee Malecela
wakitoa tuhuma hizo, makundi mbalimbali ya Jumuiya ya Vijana UVCCM nao
wameibuka na kumshutumu Makonda kuwa aliyoyasema ni maoni yake na siyo
msimamo wa Jumuiya hiyo.
Kauli hiyo ya Makonda imeibua
malumbano baina ya viongozi wa jumuiya hiyo, wengi wakimshutumu kwa
"kutumiwa kumchafua Lowassa" na kwamba kauli aliyoitoa ni ya kwake na
idara yake, wala isihusishwe na Umoja wa Vijana wa CCM.
Baadhi ya waliojibu ni pamoja na
wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kupitia kundi la vijana, Jonas
Nkya na Ramadhani Kimwaga, pamoja na Mjumbe wa Baraza Kuu la jumuiya
hiyo Mkoa wa Mbeya, Adam Mwakalinga.
Vijana hao kwa nyakati tofauti
wanasema wamehuzunishwa na matamshi ya Makonda akimshutumu Lowassa na
kutamka kuwa umoja huo hautaki kuingizwa katika masuala binafsi ambayo
yanaweza kukigawa chama na jumuiya zake.
Mwakalinga anasema Makonda anapaswa
kufanya kazi ya idara yake ya watoto badala ya kukurupuka na kutaka
kuwaaminisha Watanzania kuwa Edward Lowassa si kiongozi mzuri huku
akijua wananchi wenyewe na hata wapinzani wanaona uthubutu wake katika
maendeleo hasa kwa vijana.
Kauli ya Sadifa
Kauli ya Sadifa
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM), Sadifa Juma Khamis anasema kutangaza nia ya kugombea nafasi
yoyote ndani ya chama si kosa mradi tu mhusika ataridhika kuwa na nia,
sifa na uwezo wa kile anachokisema.
Anasema ingawa UVCCM haijakaa kujadili
watu hao, lakini haoni kosa lolote kwa mwanaCCM kujitokeza na kutangaza
nia yake hadharani.
"Nikuulize mwandishi, kutangaza nia ni
kosa? Kama mtu ameamua kueleza nia yake anakuwa amevunja sheria
gani...sioni kosa lolote endapo mtu ameeleza nia yake baada ya kujiona
anazo sifa, uwezo hiyo ni haki kikatiba," alisema
Hata hivyo, Sadifa anasema kosa
analoliona na ambalo ni kinyume na kanuni za chama ni kwa mtu
kujipitisha na kuanza kusaka kuungwa mkono ingawa alikiri kuwa kwa yeye
kama mwenyekiti hakuna aliyejitokeza kuomba amuunge mkono.
Anaongeza kusema kuwa kauli iliyotolewa na Makonda si ya Jumuiya kwa kuwa UVCCM haimuungi mkono mgombea yeyote.
"Msemaji wa UVCCM ni mmoja kitaifa na
ndiyo mimi, hakuna msemaji mwingine...yaliyosemwa na Makonda ni yake
mwenyewe na siyo msimamo wa jumuiya," anasema.
Anaongeza kuwa ingawa Makonda anayo
haki ya Kikatiba kutoa maoni yake lakini siyo sahihi wala busara kwa
mwanachama kumsema mwanachama mwingine hadharani, badala yake mambo hayo
yangepaswa kujadiliwa kwenye vikao vya ndani vya chama.
Wito kwa wanaCCM
Sadifa anatoa wito kwa makundi yote
yanayoibuka na yaliyopo ndani ya chama hicho kutulia kwa kile alichosema
muda wa kampeni haujafika na kwamba hali hiyo ikiendelea itasababisha
chama kushindwa kumpata mgombea safi maana wote watakuwa wameshachafuka.
"Ushauri wangu ni kwa wanaCCM wote
kuwa watulivu kwa faida ya chama...kuchafuana au kuharibiana ni
kukiharibia chama kwani wakati ukifika tutashindwa kumpata mgombea
safi," anasema Sadifa.
Kauli ya Msekwa
Wakati malumbano hayo yakiibuka,
Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa anawaonya wanachama wa
chama hicho wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu
ujao kuzingatia kanuni za chama hicho, vinginevyo watahukumiwa kwa
mujibu wa kanuni zenyewe.
Msekwa anasema kutangaza nia kabla ya
wakati ni kukiuka kanuni za chama ambazo zinaeleza wazi kuwa wagombea wa
nafasi mbalimbali watajitangaza baada ya chama kutoa ratiba yake.
Anasema CCM inaongozwa kwa mujibu wa
kanuni na katiba yake na kwamba katika jambo hili linaloibuka sasa
kanuni ndiyo zinayohusika ambazo zinaeleza wazi mgombea afanye nini na
kwa wakati gani.
"Mimi mwenyewe nilishiriki kuandika
hizi kanuni, utakapofika wakati, chama kitatoa ratiba yake na kila
mwenye nia atakuwa na uhuru wa kueleza nia yake, lakini kutangaza
kugombea sasa kabla ya wakati ni kukiuka kanuni za chama na ni kosa
kubwa," anasema Msekwa.
Msekwa anatoa angalizo kwa wale
wanaodhani kuwa kwa kuvunja kanuni wanakivuruga chama, badala yake
wahusika wanafanya makosa yatakayowaathiri wenyewe.
Hii si mara ya kwanza kwa Msekwa
kukemea makundi ndani ya chama hicho, akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM,
wakati akiwahoji watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho, alipata
kusema makundi ya wanaowania urais, yanakivuruga chama na kuwa
hakitawavumilia wanaochochea migogoro hiyo kwa masilahi yao binafsi.
Chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment