ADV

ADV

ADVERTISEMENT CORNER

HUDUMA YA KUKATA TICKET ZA NDEGE ONLINE


SOMA HABARI

SOMA HABARI

Thursday, March 12, 2015

Nape: Dk. Slaa ni Muongo na Mzushi aliyebobea Kiasi cha Kuitwa Dokta .........Aanika Maovu yake yote Amtaka amrudie Mwenyezi Mungu Haraka



Tarehe 08/03/2015, Dr. Wilbroad Slaa Katibu Mkuu wa Chadema kupitia kwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Ndugu Mabere Marando alitoa tuhuma kwa Serikali na kuwahusisha baadhi ya viongozi wa juu wa CCM kuwa wanapanga njama za kumdhuru Katibu Mkuu huyo wa Chadema.

Kimsingi tuhuma hizi ni za kipuuzi, lakini uongo huu usipojibiwa unaweza kugeuzwa kuwa ajenda na Chama hiki cha Chadema kwa kukosa ajenda zingine za maana. Hakuna asiyejua kuwa Chadema kwa sasa kinapumulia mashine, hivyo maneno na matendo yao kwa sasa lazima yalenge kujaribu kujinasua na balaa la kufa kwa chama chao.

Ni vizuri Watanzania wakakumbuka historia ya tuhuma lukuki zilizowahi kutolewana Katibu Mkuu huyu wa Chadema toka aanze siasa na ambazo zote zilikuja thibitika kuwa ni za uongo. Hapa nitawakumbusha baadhi.


Akiwa Singida katika kampeni za Urais za mwaka 2010,Dk. Slaa aliwatangazia wananchi mkutanoni kwamba kulikuwa kumekamatwa lori kubwa la mizigo (semi-trela) lililojazwa karatasi za kura za Urais zilizokuwa tayari amepigiwa kabisa mgombea Urais wa CCM, Dk.Jakaya Kikwete. Katika kuonyesha kwamba alikuwa na uhakika wajambo hilo, alisoma hadi namba za lori hilo na tela lake kutoka kwenye karatasi aliyokuwa ameshika mkononi, kisha akasema kuwa lori hilo lilikamatwa katika mji mdogo wa Tunduma, mkoa wa Mbeya wakati likiingia nchini kutoka Lusaka, Zambia.
Lakini baada ya polisi kuchukua hatua za haraka wakitumia namba za lori na tela lake alizokuwa amezisoma na kulikamata, kisha wakalipekua hadharani huku wananchi wakishuhudia palepale Tunduma, kilichokutwa ndani ya lori ilikuwa shehena ya vipodozi vya kina mama na sabuni za manukato.Baada ya siku chache huku akiwa amesahau yote, Dk.Slaa akatangaza tena kuwa mgombea Urais wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alikesha katika hoteli ya Lakairo, Mwanza akiweka mikakati ya kuiba kura siku ya uchaguzi huo wa mwaka 2010 ili ashinde. Siku chache alisema kura zimeingizwa na zimeshapigwa, hapa amesahau anadai ndio kwanza mpango unapangwa.

Aliwataja watu wengine aliodai walikuwa pamoja na Rais Kikwete kuwa ni aliyekuwa Mbunge wa Igunga,Rostam Aziz na Mkurugenzi wa Hoteli hiyo iliyopo katika jiji la Mwanza, Lameck Airo.

Lakini wakati Dk. Slaa akisema uongo huo,Rais Kikwete siku nzima na usiku wake wote alikuwa Mtwara akiendelea na kampeni zake za Urais.

Hata Rostam Aziz naye kwa siku hiyo pamoja na usiku wake wote alikuwa Igunga akiendelea na kampeni zake za Ubunge, na pia hata Airo naye siku nzima na usiku wote huo alikuwa jimboni kwake Rorya akifanya kampeni zake za kugombea Ubunge.

Baada ya kushindwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk. Slaa aliwaambia waandishi wa habari kwamba alikuwa na ushahidi wa matokeo ya Urais ya kituo kwa kituo ya nchi nzima yakionyesha kuwa alishinda.

Akasema, chama chake kingeyasoma hadharani na kuwakabidhi waandishi wa habari ili wananchi waujue ukweli kuwa alidhulumiwa ushindi wake, kazi iliyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na haki yake akapewa aliyekuwa mgombea Urais wa CCM, Jakaya Kikwete.

Lakini kwa vile alikuwa akiwatangazia uongo wananchi, Dk. Slaa hadi leo hajawahi kuyasoma matokeo hayo ya kughushi, badala yake alipowaita tena waandishi wa habari akatangaza kuwa Tanzania isingetawalika mpaka arudishiwe haki yake. Hapo ndipo ghasia zikiwemo za mauaji za Chadema zilipoanza hadi leo.
Januari, 2011 aliwaambia waandishi wa habari kwamba alikuwa na mkanda unaothibitisha kuwa mauaji ya Januari 5, mwaka huo yaliyofanyika katika jiji la Arusha kutokana na maandamano ya vurugu ya wafuasi wa Chadema yalifanywa kwa makusudi na polisi, na kwamba wafuasi wake hawakufanya fujo wala vurugu zozote.

Alisema mkanda huo angeuonyesha mbele ya waandishi wa habari ndani ya siku tatu au mbili baada ya Polisi Makao Makuu,kuonyesha unaothibitisha kwamba wafuasi wa Chadema walifanya vurugu ikiwemo kutaka kuvamia Jengo la Makao Makuu ya Polisi la Mkoa na kupora silaha zilizokuwa humo, wawafungulie wahalifu waliokuwa ndani na kulichoma moto jengo lenyewe.

Lakini tokea kipindi hicho hadi sasa ikiwa tayari imeshapita miaka minne, Dk. Slaa siyo tu ameshindwa kuuonyesha mkanda huo “ndani ya siku tatu ama mbili” alizokuwa ameahidi, bali amethibitisha kwamba alichosema kwa Watanzania ulikuwa ni uongo na uzushi.
Mwaka 2011, Dr. Slaa alikwenda mbali kwa kuzusha kwenye mkutano wa hadhara kuwa aliyekua Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga wakati huu Brig. Gen. mstaafu Yohana Balele amefariki dunia.

Akajaribu kuwaaminisha wananchi pale kuwa ni kweli, baadae ikagundulika kuwa Mkuu huyo wa Mkoa ni mzima na wala haumwi. Haikujulikana mara moja sababu za Dr. Slaa kumzushia kifo Mkuu huyo wa Mkoa.
Julai 2012, Dr. Slaa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika walizusha kwamba wanafuatiliwa na baadhi ya Maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa ili wauawe, lakini walipotakiwa kupeleka ushahidi wao katika vyombo vya dola ili kusudi watuhumiwa wachunguzwe na hatimaye wakamatwe na kuruhusu Sheria ichukue mkondo wake, wote waligoma na kudai hawapo tayari kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Waliendelea na msimamo huo hata pale Dk. Slaa alipolazimishwa kwenda Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na kuhojiwa, lakini akashindwa kutoa uthibitisho wake mwenyewe wala wa Mnyika kwa sababu walidai suala hilo limezungumzwa katika kikao cha Kamati Kuu ya Chadema.
Mwaka 2012, Dr. Slaa akiwa ziarani Ifakara wilayani Kilombero mkoa wa Morogoro, alidai kuwa CCM imeingiza silaha kutoka nje ya nchi kontena zima, ili zitumike kuwadhuru viongozi wa Chadema, jambo ambalo hata hivyo hadi leo ameshindwa kulitolea uthibitisho wala kielelezo chochote.

Wanaomfahamu vizuri endapo ingekuwa kweli angeita waandishi wa habari, akatoa ushahidi wake na kuwakabidhi ili wautumie kuandika madai hayo, lakini kwa sababu ulikuwa ni uongo ndiyo maana hakutoa karatasi yoyote hadi leo.
Juzi bila aibu anaibuka na tuhuma zingine za eti kutaka kuuawa. Kupanga kumdhuru Dr. Slaa, ili CCM ipate nini kwa kudhurika kwake? Kwa umri wake, afya yake na kadhalika, kwa nini CCM ipange kumdhuru mzee huyu? Huu ni mwendelezo wa tabia yake ya kuzusha mambo ya uongo kila anapoona anachuja kisiasa. Ni busara kwa umri wake akatumia muda wake mwingi KUMRUDIA MWENYEZI MUNGU.



Lakini hata mtu aliyetumika kuufikisha uongo huo kwa umma, naye ana historia ya kuzusha mambo na kusema hata asiyoyaamini.

Marando aliwahi kuitisha kikao na waandishi wa habari na kudai Katibu wa Itikadi na Uenezi alifaidika na pesa za EPA, alipobanwa na mteja wake aliyekuwa akimtetea mahakamani kwa kesi hiyo hiyo ya EPA, akaruka yale matamshi yake kwa maandishi na kudai ilikuwa ni shinikizo la Chama chake kusoma yale maneno lakini hata yeye hayaamini.

Lakini ni Marando huyu huyu ambaye akipanda kwenye majukwaa ya siasa anadai swala la EPA ni ufisadi mkubwa sana kwa nchi na akishuka tu jukwaani, anakimbia mahakamani kwenda kuwatetea watuhumiwa hao hao wa EPA aliowaita majukwaani mafisadi wa EPA. Mzee huyu naye ni MNAFIKI.

Hebu tujiulize, ni lini Mabere Marando aliacha rasmi kazi yake ya awali ya ukachero mpaka aaminike leo kufanya kazi afanyayo? Nani alimtumia kujaribu kusambaratisha chama cha NCCR-Mageuzi miaka ya mwanzo ya mfumo wa vyama vingi nchini? Hivi ni kweli Marando ni wa kuaminiwa leo?

Natoa wito kwa Watanzania bila kuingilia utaratibu wa Sheria na vyombo vya Serikali kufuatilia uongo huu mpya, Watanzania nawaomba wampuuze na kupuuza uongo huu. Usitupotezee muda, tuendelee na mambo ya msingi ya kujenga nchi yetu.

Nimshauri pia BABU yangu Dr. Slaa, kwa umri wake, wenzake wakifikisha umri huu wa uzee wanatumia muda wao kumrejea Mwenyezi Mungu badala ya yeye kuendelea kutunga uongo na uzushi kila kukicha. Namwomba mwenyezi Mungu amuwezeshe kuiona busara hiyo.

Imetolewana:-


NapeMoses Nnauye,

KATIBUWA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
ITIKADINA UENEZI10/03/2015

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...