MAWAZIRI wote wamezuiwa kusafiri kikazi nje ya Jiji la Dar es Salaam
kutokana na kile kinachoelezwa ni maandalizi ya kukabidhi ofisi kwa
mawaziri wapya ambao wanatarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa.
Taarifa hizo zimekuja siku moja tu tangu Ikulu kupitia kwa Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salvatory Rweyemamu, kuwataka Watanzania
kuwa na subira kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete wakati wowote kuanzia sasa
atatoa uamuzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo.
Profesa Muhongo na baadhi ya viongozi wengine wa Serikali, wanahusishwa
na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya
Tegeta Escrow.
Jana, vyanzo mbalimbali vya habari serikalini, vililidokeza MTANZANIA
kuwa mawaziri wote sasa wamezuiwa kusafiri nje ya Dar es Salaam kutokana
na kusubiri mchakato huo wa kukabidhi ofisi.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, karibu mawaziri wote na naibu mawaziri
walikuwapo jijini Dar es Salaam jana isipokuwa wachache ambao
haikuthibitika mara moja kama walikuwapo au la.
Vyanzo hivyo viliongeza kwamba tayari Rais Kikwete amekwishamaliza
mchakato wa uteuzi na baraza jipya la mawaziri, ikiwa yupo nchini Uswisi
katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Dunia.
“Ni kweli tumepokea maagizo ya kutosafiri nje ya Dar es Salaam, lakini
kwa hili ni hofu tupu, si suala la mabadiliko madogo ya kawaida kama
Bunge lilivyoazimia.
“Nina hofu huenda Rais Kikwete anataka kufanya mabadiliko makubwa kwa
baraza lote la mawaziri, acha tusikilize hadi mwisho nini kitaendelea
maana ni presha tupu sasa,” kilisema chanzo chetu.
Kwa miezi miwili sasa nchi imegubikwa na mjadala kwa watu wa kada
tofauti kushinikiza kufanyika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri baada ya
Bunge kupitisha maazimio manane likiwamo la kutaka kufutwa uteuzi wa
mawaziri waliotajwa kuhusika na sakata la uchotwaji wa fedha katika
Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT).
Mawaziri wanaotakiwa kuwajibishwa kwa kufutwa uteuzi wao kutokana na
maazimio hayo, ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo pamoja na
Profesa Anna Tibaijuka ambaye tayari Rais Kikwete alitangaza kufuta
uteuzi wake wa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Desemba
22, mwaka jana.
Viongozi wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim
Maswi ambaye amesimamishwa kupisha uchunguzi, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye amejiuzulu.
Juzi katika mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya
Rais Ikulu, Rweyemamu, alisema taratibu za kumwajibisha Profesa Muhongo
kama kiongozi wa kisiasa hazifanani na hatua zilizochukuliwa kwa Katibu
Mkuu wa wizara hiyo, Maswi kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Serikali.
Akizungumzia ziara za Profesa Muhongo anazoendelea nazo mikoani,
Rweyemamu alisema tuhuma hizo hazimzuii kufanya kazi kwa kuwa bado
hajaondolewa kwenye nafasi ya uwaziri aliyonayo.
Desemba 22, mwaka jana, Rais Kikwete akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar
es Salaam, alisema amemuweka kiporo Profesa Muhongo maana bado hajapata
ufafanuzi kuhusu mambo kadha wa kadha, na kwamba baada ya siku mbili,
tatu hivi atakapopata ufafanuzi na kujiridhisha, atachukua uamuzi.
Siku nne baadaye, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alinukuliwa
na vyombo vya habari akisema Rais Kikwete bado hajakamilisha
kulishughulikia suala hilo na kwamba litakapokuwa tayari wananchi
watajulishwa hatua alizochukua.
Ikiwa Rais Kikwete atafanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, itakuwa ni
mara ya nne kufanya hivyo tangu aingie madarakani mwaka 2005.
Kwa mara ya kwanza alifanya mabadiliko mwaka 2008 baada ya aliyekuwa
Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa kujiuzulu kutokana na sakata
la Richmond.
Mei 4, mwaka 2012 Rais Kikwete alifanya tena mabadiliko makubwa ya
Baraza la Mawaziri baada ya Bunge kutaka mawaziri wanane waliotajwa
kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
Ludovick Utouh wawajibike au wawajibishwe.
Mawaziri waliotakiwa kuwajibishwa baada ya kushindwa kuwajibika ni
Mustafa Mkulo aliyekuwa Waziri wa Fedha, Omary Nundu (Uchukuzi), Dk.
Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Profesa Jumanne Maghembe
(Kilimo, Chakula na Ushirika), Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara),
George Mkuchika (Tamisemi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii) na
William Ngeleja (Nishati na Madini).
Kwa mara ya tatu, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri
Januari 19, 2014 baada ya kutengua uteuzi wa mawaziri wanne kufuatia
ripoti ya Bunge kubaini kuwapo vitendo vya ukiukwaji wa haki za
binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji, utesaji na udhalilishaji vikidaiwa
kutendwa na watekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Ripoti hiyo ya kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira,
ilieleza kuwa athari zilizotokana na operesheni hiyo zilisababishwa na
wizara nne zilizokuwa zikiongozwa na mawaziri hao.
Waliong’olewa katika sakata hilo ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na
Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David.
Source: Restlink