ADV

ADV

ADVERTISEMENT CORNER

HUDUMA YA KUKATA TICKET ZA NDEGE ONLINE


SOMA HABARI

SOMA HABARI

Wednesday, March 25, 2015

WIZARA YA NISHATI NA MADINI YATANGAZA UFADHILI WA MASOMO NCHINI CHINA KWA MWAKA 2015


 Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud akizungumza na wanahabari.

  Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi, kuhusu ufadhili wa masomo nchini China kwa mwaka 2015. Kulia ni Ofisa Habari wa Maelezo, Fatma Salum.

 Mwanahabari Salome Kitomari kutoka gazeti la Nipashe, akiuliza maswali katika mkutano huo.

 Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.

Hapa mkutano ukiendelea.
Na Dotto Mwaibale
WIZARA ya Nishati na Madini imetangaza nafasi za masomo kwa vijana wa Tanzania kwa ufadhili wa Serikali ya Watu wa China kwa kipindi cha mwaka 2015.

Hayo yalibainishwa na Msemaji wa Wizara hiyo Badra Masoud Dar es Salaam leo wakati akizungumza na wanahabari.

Alisema nafasi hizo za masomo ni ngazi ya Shahada ya Juu ya Uzamili katika fani ya gesi katika Chuo Kikuu cha Jiosayansi cha China ambapo muda wa kutuma maombi hayo umeongezewa hadi kufikia Machi 30 mwaka huu.

Alisema waombaji wa ufadhili huo wanatakiwa kuwa na Shahada ya Sayansi ya Ardhi au Uhandisi kutoka vyuo vinavyotambuliwa na serikali, na muombaji awe na miaka kati ya 35 na 40.

Katika hatua nyingine Masoud alisema mitambo ya kuchakata gesi imekamilika kwa asilimia 96.

Alisema kukamilika kwa mitambo hiyo inamanufaa makubwa ikiwemo umeme wa uhakika na gharama nafuu kwani utekelezaji wa mradi huo utaliwezesha taifa kuokoa trilioni 1.6 kwa mwaka zinazotumika kununua mafuta kwa ajili yua kuzalisha umeme.

Masoud  alisema kukamilika kwa mradi huu kutachochea  maendeleo ya viwanda nchini kwani viwanda vingi vimeonyesha nia ya kutumia nishati  ya gesi asilimia  katika  kuendesha mitambo  yake  ya uzalishaji.aidha umeme wa uhakika utapunguza gharama za uzalishaji na kufanya  bidhaa za tanzania kukuzika katika masoko mbalimbali duniani.

Alisema tatizo la ajira nalo litapungua kutokana na kukamilika kwa mradi huu ambao utapelekea ajira  mpya  nyingi  kupatikana na kutokana na kuwepo kwa umeme wa kutosha na uhakika katika viwanda ambapo  viwanda  vingi vitaanzishwa vilevile umeme utakwenda mashambani na kwenye biashara nyingine hivyo kwa namna moja ama nyingine ajira  zitaongezeka. 

Alisema gesi hiyo asilia pia hutumika kama malighafi katika viwanda mbalimbali kama,mbolea, kemikali,aluminiamu pamoja na kutengeneza vifaa vya plastiki uanzishaji wa viwanda vipya kutokana na matumizi ya gesi  asilimia kutachochea 

kukua kwa uchumi  wa nchi yetu na kwa upatikanaji wa ajira mpya nyingi kwa vijana wetu. 

Aliongeza kuwa Serikali kupitia wizara hiyo chini ya Mradi Endelevu wa Usimamizi wa Rasilimali Madini (SMMRP), inakaribisha maombi ya Ruzuku Awamu ya pili kwa wachimbaji wadogo nchini. 

DIAMOND MOTORS WAZINDUA GARI JIPYA LA MITSUBISHI 2015 ASX JIJINI DAR


Wema Sepetu akiwasha gari Jipya la ASX Mitsubishi katika uzinduzi wa gari hilo jijini Dar es Salaam.

Hili ndilo gari la ASX Mitsubish jipya lililozinduliwa hivi karibuni katika hoteli ya serena jijini Dar es Salaam.(P.T)

Na Mwandishi wetu Dar es Salaam
Mtangazaji wa Clouds FM, Millard Ayo na mwigizaji maarufu nchini, Wema Sepetu wamesifia gari jipya la Mitsubishi ASX la mwaka 2015 linalouzwa na kusambazwa na kampuni ya Diamond Motors (Hansa Group).
Katika uzinduzi wa kutambulisha gari hilo uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine Kampuni ya Diamond Motors wauzaji pekee wa magari kutoka Mitsubishi waliwaalika Millard Ayo na Wema Sepetu kujaribu gari hilo toleo jipya Mitsubishi ASX kabla ya uzinduzi. 
Mastaa hao walivutiwa na mwonekano wa Mitsubishi ASX lenye vioo vya kisasa juu vyenye mwanga unaomwezesha dereva na abiria kufurahia mwonekano wa pande zote.
Meneja mauzo wa Diamond Motors, Reena Ganatra alisema Gari hilo lenye luninga ndogo inayocheza DVD, iPods, Bluetooth na sauti kutoka vyanzo mbalimbali ni maalumu kwa vijana wa kisasa na familia kwani Mitsubish ASX limetengenezwa na teknolojia ya MIVEC yenye kulifanya liwe na nguvu ya 150 ps katika 6,000 rpm na nguvu ya kuzunguka kwa mwendokasi mkubwa na kwamba limetengenezwa maalum kutumia mafuta kidogo. 
“ASX ni mwanzo tu, tunazo aina nyingine za magari kama kama Pajero ambayo tunakaribia kuyatambulisha sokoni ili kuwapatia watanzania magari imara na yenye kuaminika kutoka Mitsubishi” Alisema Ganatra. 
ASX toleo la 2015 limebuniwa kwa ubora wa hali ya juu na imara likiwa na bodi gumu pia lina mfumo maalumu usiotegemea funguo hivyo kumfanya mwendeshaji kuwasha injini kwa kubofya kitufe.
“ASX kutoka Mitsubishi, imetengenezwa maalumu kukidhi mazingira ya Tanzania hasa mijini kama Dar es Salaam ambapo muda wowote dereva wa kawaida anatoka kwenye barabara nzuri na kuingia kwenye barabara zenye makorongo” alisema Ganatra
Injini ya gari hilo ambayo ni 2.0-liter imeunganishwa INVECS-III CVT inayoisaidia mwendelezo wake katika kubadili mwendo pamoja na uimara wa usukani unaosaidia mikono ya dereva kuwa salama hata anapokuwa katika mwendo mkali.
Hansa Group inayofanya biashara kama Diamond Motors Limited, imekuwa ikifanya kazi ya katika sekta ya usafirishaji tangu mwaka 1980, ikitoa huduma kwa wasambazaji na wadau wa usafiri.Kampuni hiyo huhusika na bidhaa/ huduma mbalimabali. Shughuli za Hansa Group zimesambaa karibu nchi zote za jumuia ya Africa ikitoa huduma kama vile za uchimbaji, Umeme, Mafuta na Gesi, Reli,Ulinzi, Ujenzi, Usafiri, kimataifa na jumuhia za kimataifa.

Mbaroni kwa viungo, mifupa ya albino

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe
 kamanda wa polisi mkoa wa kagere Henry mwaibambe
WATU wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera kwa kosa la kukutwa na viungo mbalimbali vya mwili ikiwemo mifupa mitatu ya mtu mwenye ulemavu wa ngozi (albino).
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Henry Mwaibambe alisema kuwa tukio hilo limetokea juzi katika kijiji cha Kyota kata ya Kimwani wilayani Muleba mkoani humo baada ya jeshi hilo kuweka mtego kwa watuhumiwa hao ambao walikuwa wanatafuta wateja wa viungo hivyo.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni James Rutozi (66) mkazi wa Kimwani ambaye ndiye aliyekuwa anahifadhi viungo hivyo na Emanueli Kaloli (50) ambaye pia ni mkazi wa Kimwani aliyekuwa anatafuta mteja wa viungo hivyo.
Alisema mara baada ya kupata taarifa kuwa kuna watu wanauza viungo hivyo kwa Sh milioni 3 waliweka pesa za mitego na kujifanya wao ni wateja na ndipo walipowakamata watuhumiwa hao wawili ambao walikutwa na mfupa mmoja na walipowabana zaidi ndipo walitoa mifupa miwili.
Alisema mnamo mwaka 2006 katika kijiji cha Rushwa kata ya Mushabago wilayani Muleba, Zeulia Jestus akiwa na miaka 24 mwenye ulemavu wa ngozi (albino) alifariki dunia muda mfupi baada ya kujifungua na ndipo watuhumiwa hao walifukua kaburi hilo mwaka 2008 kwa maelekezo ya mganga wa jadi.
Alisema pia walipotaka kujiridhisha jeshi hilo liliomba kibali mahakamani ili kufukua kaburi hilo mnamo Machi 23, mwaka huu lilipofukuliwa liligundulika kuwa viungo hivyo vimetolewa katika mwili wa marehemu huyo.
Aidha, jeshi hilo linamtafuta mganga wa jadi aitwaye Mutalemwa Revocatus ambaye ametoroka kabla hajakamatwa ambaye ndiye aliyewashawishi wafukue hilo kaburi na kuwapa dawa ya kinga ili wasidhurike wakati wanafukua.
Aliongeza kuwa mnamo mwaka 2008 wananchi wa kata hiyo ya Mushabago walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuwa kaburi alilozikwa marehemu Zeulia lilifukuliwa na watu wasiojulikana baada ya kugundua tukio hilo. 

CHANZO: HABARI LEO

Tahadhari: Wanamgambo wa Kislam wa ISIL Wanapanga Kuishambulia Tanzania



Kwa mujibu wa taarifa za kiupelelezi, Dola la kiislamu la ISIL, maarufu kama Islamic state. Linampango wa kujenga himaya yake Afrika mashariki, hasa Tanzania, Ethiopia, Kenya na Somalia. Hii ni kutaka kuungwa mkono na kujitanua zaidi kwenye nchi za Afrika. Pia Dola hilo limekuwa likipanga kuishashambulia Tanzania, hasa miji ya Mwanza na Dar Es Salaam.



Sakata la Urais, January Makamba Amlipua Lowassa,


January Makamba Amfungukia Lowassa.
 "Nafasi ya Urais ni nafasi ya hadhi na heshima kubwa. Unapoiomba hupaswi kufanya michezo ya kuigiza. Huu utaratibu wa kuratibu watu, kuwasafirisha, kuwapa posho na ubwabwa waje kukuomba kugombea ni michezo ya kuigiza ambayo ni aibu kubwa.
Kila mgombea ana uwezo wa kutengeneza WATU wa kumuomba kugombea lakini wengine hatufanyi hivi kwasababu tunaheshimu nafasi tunayoiomba na tunaamini kwamba haipaswi kutafutwa kwa ulaghai na maigizo.
Ni aibu sana kutumia shida na njaa za watu kisiasa. Ni aibu sana kukusanya vijana na wazee wa watu na kuwapangia viti na mahema na kuwapa pesa halafu pesa na kuwapiga picha. Ukiona mtu anatafuta nafasi ya uongozi kwa ujanja na ulaghai ujue atatawala kwa ujanja na ulaghai.
Viongozi wanaokubalika na watu hawangaiki kupanga Viti na mahema na kuwapiga picha watu wanaowakubali.

Mgombea anayehaha na kutumia pesa nyingi kuonyesha anakubalika ukweli ni kwamba hajiamini. Kama unakubalika huwezi kuratibu makundi na kuyalipa na kuwapiga picha na kuita waandishi wa habari waje kushuhudia. Hizo ni mbinu za mfa maji.

Naamini Chama changu hakitatishwa na nguvu za maigizo. Tunataka uongozi safi unaomuogopa mungu. Tunataka uongozi wenye uadilifu na fikra mpya za kuisogeza mbele Tanzania. Tunataka viongozi watakaomaliza shida za Watanzania sio wanaozitumia shida hizo kisiasa
Hata Mzee Makamba, pamoja na umri wake wa miaka 75, leo akiwa na pesa za kumwaga anaweza kutengeneza makundi yakamuombe kugombea Urais.

Ifike mahali katika nchi yetu tuache hii michezo. Tukiendelea na mambo haya, tunatengeneza taifa linaloendeshwa kwa propaganda tu. Watu wanaotaka kuomba nafasi ya Urais wanapaswa kuwa na ujasiri na wanapaswa kujiamini na kusema wanataka nafasi hiyo na wana fikra gani mpya bila kutumia pesa kuonyesha kwamba wanagombea kwasababu wanahitajika na watu. Uongozi thabiti na shupavu hautokani na michezo ya kuigiza."
January Makamba.

Tuesday, March 24, 2015

BONDIA MCHINA AWASILI Dar Es Salaam.

Rais wa oganaizesheni ya ngumi za kulipwa nchini TPBO Yassini Abdalla kushoto akisalimiana na bondia Wang Xin Hua kutoka China mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Dar es salaam jana kwa ajili ya mpambano wake na mohamed Matumla utakaofanyika march 27 katika ukumbi wa diamond jubilee katikati ni Rais wa ngumi za kulipwa nchini PST Emanuel Mlundwa na kulia ni promota wa mpambano uho Jay Msangi.
Rais wa oganaizesheni ya ngumi za kulipwa nchini TPBO Yassini Abdalla kushoto akisalimiana na bondia Wang Xin Hua kutoka China mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Dar es salaam jana kwa ajili ya mpambano wake na mohamed Matumla utakaofanyika march 27 katika ukumbi wa diamond jubilee katikati ni Rais wa ngumi za kulipwa nchini PST Emanuel Mlundwa.
bondia Wang Xin Hua kutoka China
Bondia Wang Xin Hua kutoka China akilakiwa na mwenyeji wake Rais wa ngumi za kulipwa nchini PST Emanuel Mlundwa

KINANA AWATAKA VIONGOZI WEZI, MAFISADI KUNG'OKA HARAKA CCM

 Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na msafara wake ukiwa umezingirwa na wananchi wa jamii ya kimasai ulipokuwa ukiondoka baada ya kuhutubia mkutano katika Kijiji cha Mtakuja, Kata ya Kia, Jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro leo, wakati wa ziara ya kuimarisha uhai wa chama, kukagua miradi inayotekelezwa kwa kufuata Ilani ya Uchaguzi ya CCM, pamoja na kusikiliza kero za Wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

Komredi Kinana ambaye katika ziara yake ameambatana na Katibu wa Itikadiu na Uenezi, Nape Nnauye, ameutaka uongozi wa Kampuni ya Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro kuacha kuwabughudhi wananchi wa kata hiyo, baada ya kutoa mallamiko kuwa unataka kuwapora ardhi iliyo karibu na uwanja huo yenye ukubwa wa zaidi ya hekali 10,000 inayomilikiwa na vijiji 11.

Komredi Kinana amekemea tabia hiyo ya baadhi ya viongozi wanaopora kinguvu ardhi za wananchi. Pia amewahakikishia wananchi hao kuwa atasaidia kurejesha ardhi hiyo kwa kukutana na Rfais Jnakaya Kikwete na kumwambia juu ya dhulma hiyo/

Komredi Kinana , amesema kuwa kiongozi yeyote aliyeingia CCM kwa minajiri ya kutaka kujineneemesha binafsi kimaisha, kwanzia sasa hatakuwa na nafasi na inabidi aondoke katika chama hicho ambacho kazi yake ni kutetea haki za wanyonge.
 Komredi Kinana akishangiliwa na wananchi wa Kijiji hicho cha Mtakuja kinachokaliwa na jamii ya wamasai.
 Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akishangiliwa na wananchi wa Kata ya Kia katika mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Mtakuja.

 Wananchi wakishangilia baada ya kufurahishwa na hotuba ya Komredi Kinana.
 Wananchi wa Kata ya Kia, wakimpatia zawadi ya vazi la Kimasai pamoja na fimbo, Komredi Kinana wakati wa mkutano huo.
 Komredi Kinana akihutubia katika mkutao wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mtakuja, Kata ya Kia, Jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro.
 Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akihutubia mkutano wa hadhara mjini Hai leo. Jimbo hilo linaongozwa na Mbynge, Freeman Mbowe wa Chadema. Amesema mbunge huyo ajiandae kuachia jimbo hilo kwani katika uchaguzi wa mwezi Oktoba CCM mwaka huu itashinda kwa kishindo na kutwaa jimbo hilo
 Wananchi wakisikiliza kwa makini hotuba ya Komredi Kinana mjini Hai wakati wa mkutano wa hadhara.
 Waziri wa Elimu wa zamani, ambaye pia alikuwa waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Israel Nawinga, akimueleza jambo Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alipotembelewa na viongozi wa CCM kumjulia hali nyumbani kwake Losaa, Masama wilayani Hai leo.
 Komredi Kinana akishiriki kuchimba msingi wakati wa ujenzi mpya wa majengo ya Shule ya Msingi Modio iliyopatwa na jangoa la tetemeko na kubomoka eneo la Masama Mashariki, wilayani Hai.
 Watoto wanaosoma Shule ya Awali wakipita bila woga kwenye Daraja la zamani sana la Mnepo liliotengenezwa kwa kamba za waya katika Kijiji cha Kiyungi, wilayani Hai.
 Mmiliki wa Blogu hii, Kamanda Richard Mwaikenda akipita kwa uangalifu kwenye Daraja la zamani la Mnepo, wilayani Hai, Kilimanjaro leo.
 Komredi Kinana akishiriki kupaka rangialiposhiriki ujunzi wa daraja jipya la Mnepo lililojengwa kwa fedha za Serikali takribani sh. bilioni 1 katika Kijiji cha Kiyungi mpakani mwa wilaya za Hai na Moshi Vijijini.
 Komredi Kinana akikagua ujenzi wa Daraja jipya la Mnepo
 Komredi Kinana akipita kwenye daraja la zamani la Mnepo lililojengwa enzi za ukoloni katika Kijiji cha Kiyungi, mpakani mwa Wilaya za Hai na Moshi Vijijini. Daraja hilo limejengwa na kwa waya.
 Komredi Kinana akimkabidhi ng'ombe iliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kwa Kijiji cha Kwasadala kilichofanya vizuri katika uchaguzi uliopita hivyo kuipatia CCM ushindi mnono. Pia kijiji hicho kilikabidhiwa gunia moja la mchele.
 Komredi Kinana akihutubia katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Jimbo la Hai.
 Wananchi wakipiga picha za kumbukumbu wakati Komredi Kinana akihutubia katika Kijiji cha Mtakuja, Kata ya Kia, wilayani Hai.
 Komredi Kinana akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Hai, ambapo pia alikagua ujenzi wa chumba kipya cha Xray, katika Mji wa Bomang'ombe, wilayani Hai.
 Komredi Kinana akiijaribu mitambo ya Xray iliyopo katika chumba hicho cha upimaji kwa njia ya mionzi.
 Nape akipigwa mionzi (Xray) ya mkono wake wa kulia
Wauguzi na watumishi wa hospitali ya Wilaya ya Hai, wakiwa katika picha ya pamoja na Komredi

Friday, March 20, 2015

Mkapa aponda uteuzi wa viongozi



Elias Msuya na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam
RAIS mstaafu, Benjamin Mkapa, amekosoa uteuzi wa viongozi wa umma nchini akisema sera ya utumishi wa umma inayojali utaalamu haifuatwi.
Ametoa kauli hiyo wiki chache baada ya kuzuka mjadala wa uteuzi wa wakuu wa wilaya uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete, huku ikielezwa haukuzingatia weledi, maadili na uzoefu kwa walioteuliwa.
Akizungumza katika siku ya pili ya uzinduzi wa Kavazi la Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam jana, Mkapa aliyekuwa mtoa mada, alisema kutojali taaluma ni kati ya mambo yanayorudisha nyuma maendeleo ya nchi.
“Jambo moja ninalodhani limeturudisha nyuma katika maendeleo na mnisamehe kwa kusema hili, ni sera ya utumishi wa umma.
“Tunajua kanuni za kuhamisha mtu kutoka sehemu moja kwenda nyingine, iwe ni kwa utawala wa jumla au kwenye nafasi za utaalamu. Hapa ndipo tulipopotea.
“Mzee Msuya (Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya) atakuwa amewaambia, wakati ule hata ukimaliza chuo kikuu, bado utapewa nafasi kama ofisa maendeleo ya jamii na utapitia mafunzo ili kupanda vyeo.
“Utakuwa ofisa mwandamizi au hata kamishna, lakini leo unaweza ukawa mtu yeyote na ukapangwa popote,” alisema Mkapa huku akishangiliwa na washiriki wa kongamano hilo.
Akijibu swali kama nchi za Afrika zinaweza kuendelea huku zikitegemea misaada ya wahisani, Mkapa alisema nchi zilizoendelea zina mkakati wa kuhakikisha nchi zinazoendelea haziendelei.
“Ni kweli, tunaambiwa kwamba tunashindwa kushindana na uchumi wa nchi zilizoendelea na hii ni kwa sababu wana mkakati wa kuhakikisha hatuwafikii, wanataka unyonyaji wao uendelee,” alisema Mkapa.
Akizungumzia umasikini unaolikabili Bara la Afrika, alisema jukumu la Serikali ni kuwajibika katika kuondoa umasikini wa kipato, chakula, elimu, afya, watu kushindwa kumiliki mali na kutoshiriki katika siasa.
Alisema kuwajibika kwa Serikali ni muhimu katika kujenga mfumo wa uchumi na umilikaji wa rasilimali kwa wananchi.
“Kwa sababu wananchi wengi ni wakulima wadogo na wafugaji, kigezo kikubwa cha maendeleo ni kuwamilikisha ardhi,” alisisitiza Mkapa.
Kuhusu dira ya taifa, alisema Serikali inatakiwa kuitofautisha na mipango ya maendeleo ya kila mara ili ieleweke.
Awali, akitoa mada ya kurejea kwa maendeleo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa na Afrika, Profesa Adebayo Olukoshi, alisema jukumu la Serikali duniani kote ni kupambana na umasikini wa wananchi wake.

Chama cha ACT chamwandalia Zitto makazi



  • Mbunge huyo alipanga kuliaga bunge na alisema amekwishapata ruksa ya Spika kuwa angesimama bungeni kuwaaga wabunge na wanachama wa Chadema baada ya chama hicho kumtimua uanachama wake hivi karibuni, lakini ghafla mpango huo uliyeyuka kwa kile kilichoelezwa kuwa Spika amemkatalia.



Dar es Salaam. Pamoja na mpango wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuliaga Bunge kukwama jana, Chama cha ACT- Tanzania kimetangaza kukamilisha maandalizi ya kumpokea mwanasiasa huyo kuanzia leo.
Mbunge huyo alipanga kuliaga bunge na alisema amekwishapata ruksa ya Spika kuwa angesimama bungeni kuwaaga wabunge na wanachama wa Chadema baada ya chama hicho kumtimua uanachama wake hivi karibuni, lakini ghafla mpango huo uliyeyuka kwa kile kilichoelezwa kuwa Spika amemkatalia.
Tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka mmoja uliopita, Zitto amekuwa akihusishwa kukianzisha, hivyo kitendo chake cha kujiunga nacho kitahitimisha mjadala wa muda mrefu wa mashabiki wake waliokuwa wakihoji wapi ataelekea baada ya kung’olewa Chadema.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa ACT, Samsom Mgamba aliangua kicheko na bila kuuma maneno alisema: “Hahahaa... tutampokea kuanzia kesho (leo) na maandalizi yamekamilika.”
Alipotakiwa kueleza wapi mapokezi hayo yatafanyika alisema: “Hilo mbona liko wazi, yatafanyikia makoa makuu yetu (yapo Makumbusho, Dar es Salaam) lakini kwa taarifa zaidi tutawajuza.”
Zitto anaingia ACT ikiwa ni siku tisa kabla ya chama hicho kufanya uchaguzi wake mkuu, huku akitajwa kuwa ameandaliwa kushika wadhifa wa mwenyekiti kuendeleza harakati zake za siasa.
Hivi karibuni, chama hicho kilimvua uongozi aliyekuwa mwenyekiti mwanzilishi, Lucas Limbu kutokana na mgogoro uliokuwapo baina ya viongozi na kufanya nafasi hiyo kubaki wazi.
Tayari washirika wa Zitto waliohusishwa naye kuandika waraka wa mapinduzi ndani ya Chadema na baadaye kufukuzwa uanachama, Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo wametua ndani ya chama hicho kipya.
Chama hicho ambacho kinaendelea na uchaguzi katika ngazi ya mikoa kikibakiza Mkoa wa Geita unaofanya uchaguzi wake kesho. Kitaanza vikao vyake vya kitaifa Machi 27 na kuhitimisha kwa mkutano mkuu Machi 29.
Akizungumzia uchaguzi huo, Mwigamba alisema: “Maandalizi yanakwenda vizuri na hakuna shaka utafanikiwa kwa kiasi kikubwa na tunawaomba Watanzania watuunge mkono.”
Tangu juzi, Zitto alitarajiwa kuliaga Bunge lakini hakufanya hivyo kwa kilichoelezwa kuwa aliitwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda na kupewa ushauri kuwa afanye hivyo jana jioni.
Jana asubuhi mbunge huyo hakuingika katika kikao cha Bunge lakini alionekana katika viwanja vya Bunge akiwa amevaa shati la drafti na suruali ya kaki akizungumza na rafiki yake wa karibu, Deo Filikunjombe ambaye ni mbunge wa Ludewa kupitia CCM.

Mwananchi

Hii ndio Hotuba ambayo sikuitoa jana bungeni-zitto kabwe







MAELEZO BINAFSI YA MHE. ZITTO ZUBEIR KABWE, MB KUHUSU UANACHAMA WAKE KATIKA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) NA HATMA YAKE KAMA MBUNGE KATIKA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.
DODOMA, ALHAMISI 19 MACHI 2015.
______________________________ ______
1) Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa fursa uliyonipa kutoa maelezo yangu binafsi katika Bunge lako Tukufu leo. Ninatoa maelezo haya kwa mujibu wa Kifungu cha 50 (1) cha Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013 kinachosema kwamba,

“Mbunge yeyote anaweza, kwa idhini ya Spika, kutoa maelezo binafsi Bungeni yanayolenga kufafanua kuhusu jambo lolote linalomhusu na lililoifikia jamii”

2) Mheshimiwa Spika, Nilijiunga na Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza Mwaka 2015 nikiwa na lengo kuu la kupaza sauti ya vijana kwenye masuala yanayohusu nchi yetu na kutetea maslahi ya Watanzania hususani Wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Mkoa wa Kigoma, na Watanzania kwa ujumla. Nilichaguliwa na wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Wananchi wa Kigoma Kaskazini walinichagua tena Mwaka 2010 kupitia tiketi ya CHADEMA.

3) Mheshimiwa Spika, kupitia fursa ya ubunge niliyopewa na wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa udhamini wa CHADEMA, nimejifunza mengi hapa Bungeni na nje ya Bunge hili. Nimeijua nchi yangu, nimejua siasa na nimejulikana ndani na nje ya Tanzania. Muhimu zaidi ni kwamba nimepata fursa adhimu ya kutoa mchango wangu katika kutunga sheria na sera mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Aidha, nilipata fursa ya kipekee kama Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati zako mbili ya kuisimamia, kuishauri na kuiajibisha serikali.

4) Mheshimiwa Spika, Ninawashukuru sana wanachama wa CHADEMA kwa dhamana mbalimbali walizonipa ndani ya CHADEMA. Ninawashukuru viongozi wangu na hasa Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kunilea na kuniamini kufanya naye kazi kwa kipindi chote tangu nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika chama na hapa Bungeni. Kama ambavyo nimesema mara nyingi, CHADEMA imenilea na kunikuza tangu nikiwa na umri wa miaka 16 na tangu kipindi hicho nimejifunza mengi.

5) Mheshimiwa Spika, Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa mapenzi yao na imani waliyonipa na kuniwezesha kukalia KITI hiki ninachokalia ndani ya Bunge lako Tukufu. Nashukuru kwamba juzi nilipata fursa ya kipekee ya kuwashukuru kwa imani waliyonipa kuwatumikia kwa vipindi viwili mfululizo. Mola atawalipa wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa imani kubwa walioionyesha kwangu na kuniwezesha kulitumikia Taifa langu kwa namna nilivyolitumikia.

6) Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa pamekuwa na msuguano wa kiuongozi kati yangu na viongozi wangu ndani ya CHADEMA uliosababishwa na tofauti za kimtazamo juu ya tafsiri pana ya demokrasia ndani ya chama chetu. Hatimaye tofauti hizi zilipelekea mwezi Novemba 2013 Kamati Kuu ya CHADEMA kunivua nafasi zangu zote za uongozi nilizokuwa nazo. Sikuridhika na maamuzi hayo na hivyo nikaonyesha kusudio la kukata rufaa katika Baraza Kuu la chama chetu kama taratibu za kikatiba za chama chetu zinavyotaka. Bahati mbaya ofisi ya Katibu Mkuu haikunipa fursa hiyo, na huo ndio ukawa msingi wa mimi kufungua kesi mahakamani kuweka pingamizi la Kikao cha Kamati Kuu kujadili hatima ya uanachama wangu hadi pale ofisi ya Katibu Mkuu itakaponipa fursa ya kukata rufaa katika vikao vya chama. Yaliyotokea baada ya hapo ni historia, lakini hatimaye Mahakama Kuu imetoa hukumu yake tarehe 10 Machi 2015. Katika hukumu hii, nimeshindwa kwa sababu za kiufundi kwa maelezo kwamba pingamizi letu liliwasilishwa kimakosa.

Pamoja na kwamba hatukuridhika na mwenendo wa jinsi kesi hii ilivyoamuliwa pamoja na maudhui ya hukumu yenyewe, ninaheshimu maamuzi ya mahakama na sina mpango wa kukata rufaa.

7) Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida na kwa mujibu wa katiba ya chama chetu, ilitarajiwa kwamba baada ya maamuzi ya Mahakama Kuu, Kamati Kuu ingekaa na kunipa rasmi mashtaka yangu yanayohusu uanachama wangu, mimi kuitwa kujieleza na hatimaye Kamati Kuu kutoa uamuzi wake. Hata hivyo, mara baada ya hukumu ya Mahakama Kuu dunia nzima ilitangaziwa na Mwanasheria wetu Mkuu, kwa niaba ya chama, kwamba mimi nimeshafukuzwa na sio mwanachama tena wa CHADEMA. Baada ya hapo viongozi wangu wametoa matamko mbalimbali yote yakionyesha kwamba sitakiwi tena katika chama hiki, pamoja na kwamba hadi ninapoongea hapa leo sijawahi kukabidhiwa barua yeyote inayonitaarifu kufukuzwa kwangu katika chama.

8) Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo ya hapo juu, ni wazi kwamba uanachama wangu wa kisiasa ndani ya CHADEMA umeshaondolewa. Ninaweza kuendelea kupigania uanachama wangu kisheria na kwa kweli nina sababu na misingi yote kubaki na uanachama wangu kisheria. Lakini mimi ni mwanasiasa. Sikuja hapa bungeni kwa sababu ya kushinda kesi mahakamani. Nilichaguliwa na wananchi wa Kigoma Kaskazini na ninatambua kwamba huwezi kuwa mbunge bila udhamini wa chama cha siasa. Huu ndio utaratibu wa kisheria tuliojiwekea. Kwa mujibu wa viongozi wangu katika chama ni kwamba udhamini wa chama changu umekwishaondolewa.

9) Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo ya hapo juu, ninaomba kukutaarifu wewe na Bunge lako tukufu kwamba sina mpango wa kuendelea kupigania uanachama wangu wa CHADEMA katika viunga vya mahakama. Kwa hiyo ninatangaza rasmi leo kwamba taratibu za kikatiba zitakapokamilika tu nitaachia uanachama wa CHADEMA, chama nilichokipenda sana kwa sababu ya kuendelea kukua kwa tofauti za kiitikadi, kimtazamo na hata kibinafsi kati yangu na viongozi katika chama changu. Nimeona kuwa kuendelea kupigania uanachama kisheria ni kutatiza na kukwaza harakati za mabadiliko hapa nchini katika wakati ambapo mfumo wa kisiasa unatambua uwepo wa vyama vingi vya siasa. Kwa kuwa taratibu hizo sijui zitakamilika lini, natumia fursa hii kuwaaga wabunge wenzangu.

10) Mheshimiwa Spika, vyama vya siasa ni jukwaa muhimu katika ujenzi wa demokrasia lakini havipaswi kamwe kuwa juu ya wananchi. Kwa hiyo ni maoni yangu kwamba wakati sasa umefika wa kukomesha udola na ufalme wa vyama vya siasa hapa nchini. Mfumo wa siasa ambao unavipa vyama vya siasa mamlaka ya kisheria ya kukanyaga mamlaka ya wananchi haupaswi kuendelea katika Karne ya 21 na katika nchi ambayo inaendeshwa kwa misingi ya demokrasia ya kuheshimu wananchi. Mimi ninaondoka bungeni sio kwa sababu wananchi wangu wa Kigoma Kaskazini walionichagua wametaka niondoke. Siondoki kwa sababu nimeshindwa kufanya kazi zangu za ubunge. Na kwa kweli siondoki kwa sababu wanachama wenzangu katika CHADEMA wametaka niondoke. Ninaondoka kwa sababu mfumo wetu wa kisheria unavipa vyama vya siasa mamlaka juu ya wananchi na wapiga kura. Ni matumaini yangu kwamba Bunge lako tukufu halitaruhusu mfumo huu unaoruhusu vyama vya siasa kupora mamlaka ya wananchi uendelee. Ni Bunge lako pekee lenye uwezo wa kukomesha mfumo ambao unatukuza Parties’ Power, badala ya People’s Power.

11) Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali kwamba vyama vya siasa ni jukwaa. Bahati nzuri nchi yetu inafuata mfumo wa vyama vingi vya siasa na sasa tuna vyama 22. Kwa hivyo, wananchi wanaoniunga mkono wasisikitike kwa maamuzi yangu ya leo. Bado ninayo fursa ya kuwatumikia kupitia jukwaa lingine ambalo nitaamua katika siku chache zijazo, na inshala Mungu akitujalia nitarudi tena hapa Bungeni katika Bunge la 11 kwa nguvu za wananchi.

12) Mheshimiwa Spika, kwa miaka kumi niliyotumikia hapa Bungeni, si yote niliyoyafanya yalikuwa sahihi, yapo ambayo niliyakosea kama mwanadamu katika kufanya kazi zangu, kwa namna yeyote ile naomba radhi Watanzania wote kwa yote ambayo sikuyafanya kwa usahihi. Mimi ni binadamu, kiumbe dhaifu, sijakamilika. Ni Mola peke yake aliyekamilika.

13) Mheshimiwa Spika, siwezi kuanza maisha yangu mapya kisiasa bila ya kulishukuru Bunge lako Tukufu. Kwanza, Bunge la Tisa chini ya Mzee Samwel Sitta, mzee wa kasi na viwango! Bado ninakumbuka vizuri jinsi hoja ya Buzwagi ilivyotikisa Bunge lake na hatimaye kupelekea nchi yetu kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa sekta ya madini (Sera mpya ya Madini na Sheria mpya ya Madini ) na hivyo kukuza mapato ya sekta ya madini kutoka Tshs. 32 bilioni kwa mwaka mpaka Tshs. 450 bilioni kwa mwaka.

14) Mheshimiwa Spika, ninajivunia kuwa sehemu ya Bunge la Kumi chini yako, Mama shupavu Anna Semamba Makinda. Katika Bunge hili nimekuzwa, nimejifunza, nimepambana, nimefurahi na nimelia ndani ya Bunge hili. Kwa pamoja tumepigania maslahi ya wananchi wetu kwa juhudi na maarifa na hivyo kuleta mabadiliko kadhaa. Ni katika kipindi hiki ambapo wabunge tumekuwa na sauti. Bunge la Tisa lilijijenga likawa ‘Bunge lenye Meno’ katika kupambana na ufisadi. Bunge la Kumi limejenga ‘Bunge lenye Nguvu’ katika mfumo wa Bajeti ya nchi yetu. Kupitia Bunge hili tumeweka misingi ya kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji katika nchi yetu. Na katika siku za hivi karibuni Bunge la Kumi litakumbukwa kwa Hoja Maalumu ya Tegeta Escrow iliyopelekea mfumo wetu wa maadili ya Viongozi kupitia Baraza la Maadili kuanza kufanya kazi kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa katika miaka iliyopita.

15) Mheshimiwa Spika, wajumbe wa PAC ( ambao nimeishi nao kama familia ) tumekuwa nguzo kubwa ya kujenga uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge na wananchi. Napenda kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa kuniunga mkono na kwa kunipa ushirikiano kama Mwenyekiti wao. Changamoto na malezi mliyonipa kwa miaka yote hii yamejenga Mtanzania mmoja mwenye nia ya dhati ya kuitumikia nchi yake, muda wowote, wakati wowote na kwa namna yeyote ile bila woga wala upendeleo. Nawashukuru kwa kujitoa kwenu kwa nchi yetu na dhamira isiyo na mawaa ya kujenga Taifa imara zaidi. Pamoja na kwamba ninaondoka Bungeni leo, ninaahidi kuendelea kuwatumikia wananchi wa Kigoma Kaskazini na Taifa langu katika kusimamia ukweli, kutetea demokrasia ya kweli na kupigania maendeleo ya kweli kwa mwananchi wa kawaida bila ubaguzi wowote.

16) Mheshimiwa Spika, Kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA, najivunia kwa fursa mliyonipa kuwa sehemu ya Baraza hili la Taifa ambalo leo ninalihutubia kwa mara ya mwisho kama mbunge wa Kigoma Kaskazini. Inawezekana tusiweze kuelewana katika masuala ya uongozi, misingi na itikadi, lakini ninaamini tunapaswa kuelewana na kukubaliana katika dhamira kubwa ya kuijenga nchi yetu kuwa Taifa linalojitegemea na lisilo na aina yeyote ya ubaguzi. Taifa lenye uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira na kuondoa umasikini, ujinga na maradhi, yaani Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ni matumaini yangu kuwa tutakuwa bega kwa bega katika harakati hizi katika siku zijazo. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Nafasi hii ya kihistoria tuliyopewa haihitaji siasa za ubinafsi na unafsi! Uzalendo wetu utapimwa kwa uwezo wetu wa kuweka tofauti zetu binafsi pembeni kwa lengo lililo kubwa zaidi yetu.

17) Mheshimiwa Spika, Ninawashukuru tena na tena wana Kigoma na wananchi wote wa Tanzania ambao kwa ridhaa yao nimekaa katika viti hivi kwa miaka takribani kumi. Ninawahakikishia kuwa changamoto nilizokumbana nazo na ambazo zimenilazimisha leo niondoke bungeni zimechochea zaidi dhamira, nia na sababu yangu ya kuwatumikia kwa nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule. Huu ni mwanzo mpya.

Mheshimiwa Spika,

Asanteni sana na Kwa herini!

Mvutano kati ya UN na DRC unaendelea

Picha inaonyesha helikopta ya mashambulizi ya MONUSCO, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo.
Picha inaonyesha helikopta ya mashambulizi ya MONUSCO, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo.
Na RFI
Mvutano baina ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umechukuwa sura nyingine hapo jana katika Baraza la Usalama la umoja huo kuhusu kuondoka au la kwa vikosi vya kulinda amani nchini humo MONUSCO.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Congo Raymond Tshibanda amesema kuwa wakati umefika kwa nchi yake kuwajibika kikamilifu kwa ajili ya usalama wa nchi yake akiliomba baraza hilo kuheshimu dhamira ya serikali ya Kinshasa kwa kuamuru MONUSCO waanze kuondoka kwa awamu.
Aidha, waziri huyo amesema kuwa maendeleo ya kisiasa na kiuchumi yaliyoletwa na serikali yake ni mafanikio makubwa, huku akidai kuwa makabiliano ya vikosi vya serikali dhidi ya waasi wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR mashariki mwa DRC yanaendelea kushika kasi.(P.T)
Akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, mwakilishi maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa na mkuu wa vikosi hivyo vya MONUSCO, Martin Kobler, amesisitiza kwamba kwa ujumla hali ya usalama imeimarika na kwamba bado yako maeneo mengi ya kufanyia kazi mashariki mwa nchi hiyo ambako raia wanaishi katika hofu.
Kulingana na vyanzo vya kidiplomasia, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina mpango wa kupunguza vikosi hivyo kwa kiwango cha askari elfu mbili kati ya elfu ishirini walioko Congo wakati serikali ya Kinshasa ikisema kiwango cha kwanza cha wataokaoondoka kitakua cha askari elfu sita.

Maandamano makubwa Tunis: “Muungano wa kitaifa” dhidi ya ugaidi

Mwanamke wa Tunisia akibeba bango lililoandikwa kwa herufi za ishara ya damu mjini Tunis: " hapana kwa ugaidi" , Machi 19 mwaka 2015.
Mwanamke wa Tunisia akibeba bango lililoandikwa kwa herufi za ishara ya damu mjini Tunis: " hapana kwa ugaidi" , Machi 19 mwaka 2015.
Na RFI
Maandamano mapya yanayojumuisha mamia ya watu yanatazamiwa kufanyika Ijumaa wiki hii katika mji mkuu wa Tunisia, Tunis, mbele ya makavazi ya Bardo jijini Tunis, ambapo shambulio la kigaidi liligharimu maisha ya watu 21.
Raia wa kigeni 20 pamoja na raia mmoja wa Tunisia ni miongoni mwa waliouawa. Watu zadi ya arobaini walijeruhiwa katika shambulio hilo.
Awali maandamano kama hayo yaliandaliwa na asasi thelathini pamoja na chama kikuu cha wafanyakazi nchini Tunisia (UGTT), huku kauli mbio ikiwa " Umoja wa kitaifa"dhidi ya ugaidi.
Rais wa Tunisia Beji Caïd Essebsi, kwa upande wake ametangaza kwamba wauaji walioendesha shambulio hilo katika makavazi ya Bardo walikua walivalia " vilipuzi" na vikosi vya usalama viliwahi kuzima shambulio hilo kwa " kuepuka janga kubwa" ambalo lingeweza kutokea kutokana na vilipuzi hivyo.
Baadhi ya waandamanaji waliweka shada za maua na mishumaa kwenye eneo la tukio kwa kutoa rambirambi zao kwa wahanga.
Mokthar Trifi, kiondozi wa zamani wa shirika la haki za binadamu nchini Tunisia, ambaye alikua alishiriki maandamano hayo alisema raia wote wa Tunisia wameungana na kusema " hapana" kwa ugaidi.
Kundi la wapiganaji wa Dola la Kiislamu limekiri kutekeleza shambulio hilo dhidi ya makavazi ya Bardo mjini Tunis, lililogharimu maisha ya watu 21, wengi wao wakiwa watalii.
Washukiwa tisa walikamatwa Alhamisi wiki hii, kwa mujibu wa Ikulu ya Tunis. Watu hao wanasadikiwa kuwa walikua wakiwasiliana na wauaji hao walioendesha shambulio katika makavazi ya Bardo.

Kurasa za mbele MAGAZETI LEO JUMAMOSI

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...